Baada ya kuapishwa Jumatatu iliyopita katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, kila waziri na naibu wake wamekuwa wakiripoti katika ofisi zao huku wakiahidi mambo kemkem kulingana na sekta zilizo chini ya wizara hizo.
Miongoni mwa mabadiliko yaliyofanyika, Rais Samia alimteua Prof. Adolf Mkenda, mwanataaluma na nguli wa masuala ya uchumi, kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akichukua nafasi ya mwanataaluma nguli wa elimu, Prof. Joyce Ndalichako, ambaye amekuwa Waziri mwenye dhamana ya kazi na ajira katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Uteuzi wa Prof. Mkenda ambaye kabla alikuwa Waziri wa Kilimo, nafasi ambayo imechukuliwa na aliyekuwa naibu wake, Hussein Bashe, umeonyesha haukukosewa kutokana na dira yake katika kuboresha sekta ya elimu.
Wakati akikabidhiwa ofisi hiyo, Prof. Mkenda, alisema anatarajia kutafuta wataalamu wabobezi katika elimu, wakiwamo wastaafu ili kupata mchango wao katika maendeleo ya sekta hiyo ikiwamo uboreshaji wa mitaala.
Katika kufanya hivyo, alisema atatenga wiki tatu kuzungumza na watumishi wa wizara na kupitia nyaraka muhimu ili kufanya uchambuzi kuboresha elimu na kwa lengo la kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.
Mkenda alisema wizara hiyo ni nyeti, hivyo inatakiwa kutendewa haki kwa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na watumishi huku akiweka bayana kwamba si wizara ya kuchezea na kwamba haitakiwi kubadilisha badilisha mambo.
Kwa kauli yake hiyo na mpango wa kuwashirikisha wataalamu wabobezi na magwiji katika elimu, ni dhahiri kwamba amebaini matatizo makubwa yanayo sababisha kudorora kwa elimu na hatimaye kukwamisha mambo mbalimbali kwa maendeleo ya taifa.
Tunasema hivyo kwa sababu yako mambo mengi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa katika sekta ya elimu ikiwamo mitaala na kwamba haiendani na muktadha wa sasa wa maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na kutatua tatizo la ajira ambalo linawakumba vijana wengi ambao wanahitimu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Aidha, kwa zaidi ya miaka 20 kumekuwa na mabadiliko juu ya mitaala pamoja na mabadiliko ya viwango vya ufaulu ambavyo vimekuwa vikidaiwa kuwa ni sehemu ya mambo yanayoharibu mfumo wa elimu nchini.
Mwaka 2001 kwa mfano, mtu mmoja alipoteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni wakati huo, alitangaza kufuta mashindano ya michezo ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na ya sekondari (UMISSETA) kwa madai kwamba muda unaotumika kwa michezo hiyo hauna tija katika elimu! Pia waziri huyo huyo alifuta mtaala kwa kuunganisha Kemia, Baiolojia na Fizikia kuwa somo moja na kufutwa masomo ya biashara.
Mwingine aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na kubadilisha madaraja ya ufaulu kisha kuwa wastani wa ufaulu (GPA) kwa kidato cha pili, cha nne na cha sita. Hii ndiyo maana Prof. Mkenda anaposema elimu si jambo la kubadilisha badilisha mambo, anajua siri iliyoko ndani yake.
Kwa mantiki hiyo anaposema anataka kuwatumia hata wastaafu kupata mawazo juu ya kuleta mabadiliko ndani ya sekta hiyo, Prof. Mkenda anaonekana amedhamiria kuleta mageuzi ya elimu. Kwa hilo anastahili pongezi na aungwe mkono katika azma hiyo.