Matapeli wa kimtandao wadhibitiwe ni kero

30Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Matapeli wa kimtandao wadhibitiwe ni kero

JUHUDI zinazofanywa na Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwakamata watu wanaojihusisha na uhalifu wa kimtandao, zinatoa matumaini kutokana na uhalifu huo kuongezeka siku hadi siku.

Wahalifu wanaotumia mtandao kuwalaghai na kuwaibia wananchi hutumia mbinu mbalimbali zinazowashawishi wananchi kuingia kwenye mtego wao.

Mbinu kubwa wanayoitumia na kuwapigia wateja wa simu wa kampuni mbalimbali za mitandao hiyo na kuwalaghai watume pesa ili waongezewe salio au kwa kuwadanganya jambo ambalo mteja atashawishika kuwaamini na kuwatumia pesa.

Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), katika kudhibiti hali hiyo iliziagiza kampuni za simu nchini kusajili laini zote kwa kutumia Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na alama za vidole, lakini cha kushangaza utapeli huo unaendelea na watu wengi wanalizwa kwa kuibiwa pesa zao bila kukamatwa.

Kuna ujumbe ulizoeleka kutumwa na matapeli hao kwenye simu za watu ukisomeka ‘hiyo hela tuma kwa namba hii’ ambao kwa sasa hauonekani sana baada ya wajanja hao kubaini kuwa watu wameshawang’amua.

Kuna vijana ambao hupita mitaani kwa kuwatangazia wananchi kuwa wanasajili laini za simu, ambao hudai kutumiwa na kampuni za simu, lakini haieleweki kama usajili huo unazingatia matakwa ya TCRA.

Pengine usajili huo unaweza kuwa moja ya chanzo cha kuwapo kwa matapeli hao ambao wanaweza kusajili laini zaidi ya moja na kuzifanyia utapeli na kisha kuzitupa.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wahalifu zaidi ya 20 wamekamatwa jijini humo kwa kufanya uhalifu kwa njia ya mtandao.

Jeshi hilo linasema wahalifu hao hutumia mbinu ya kutuma ujumbe mbalimbali kupitia namba tofauti za simu wakionyesha nia ya kutaka kuwasaidia, kisha huwaibia.

Wahalifu hao walikutwa na vifaa mbalimbali wanavyovitumia kufanya uhalifu huo vikiwamo kompyuta mpakato, kompyuta za mezani, simu za aina tofauti, modemu za mitandao yote na kadi za simu za mitandao mbalimbali zaidi ya 50.

Jeshi hilo lilibaini pia mojawapo katika ujumbe wanaotumia wahalifu hao kuwaibia wananchi ni kuwadanganya wazazi kuwa watoto wao shuleni wamepata matatizo, au kuumwa sana na kutaka watume hela ili wawapeleke hospitali na wazazi wakituma wanakuwa wameibiwa.

Uhalifu mwingine ni mtu anapoibiwa simu na mwizi kutuma ujumbe kwa ndugu au marafiki wa aliyeibiwa simu awatumie pesa akidai amepatwa na tatizo kubwa. Mwizi huyo huomba kiasi kikubwa cha pesa na kama mtu hayuko makini anaweza kutuma akiamini kweli ndugu yake yuko kwenye matatizo.

Wengine hutumia mitandao ya simu kufanya mambo yasiyofaa kwenye jamii kwa kusambaza picha chafu kwa lengo la kumchafua mtu au kufanya biashara ya ukahaba kupitia njia hiyo ya mtandao.

Kazi inayofanywa na Jeshi la Polisi kuwakamata wahalifu hao itasaidia kupunguza vitendo hivyo ambavyo vimekuwa kero kwa jamii na kuharibu nia nzuri ya kuwapo kwa mitandao ya simu kurahisisha kazi mbalimbali ambazo siku za nyuma ilimbidi mtu aende moja kwa moja kupata huduma kama ya pesa au kulipia kitu.