Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Mimba na Ndoa za Utotoni Zinaepukika, Chukua Hatua Kumlinda Mtoto wa Kike”. Maaadhimisho hayo yanafanyika huku takwimu zikionyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya mimba za utotoni.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) mwaka 2010 zinaonyesha wastani wa kitaifa asilimia 37 na mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni ya Shinyanga, asilimia (59), Tabora (58) na Mara asilimia (55). Utafiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), ulionyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012/13, matukio 228 ya mimba za utotoni na matukio 42 ya ndoa za utotoni yaliripotiwa.
Katika kupambana na hali hiyo, jamii yetu inapaswa kujua ni sababu zipi zinachangia hali hiyo. Hata hivyo, kumekuwapo na taarifa za utafiti kwamba Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ndiyo kichocheo kutokana na kueleza kwamba mtoto wa miaka 14 anaweza kuolewa kwa ruhusa ya wazazi.
Udhaifu wa sheria hiyo umekuwa ukitumiwa vibaya na wazazi kadhaa ambao kutokana na tamaa ya kupata fedha, wamekuwa wakiwaoza watoto wao kwa ajili ya kupata mali itokanayo na mahari wanayopokea.
Kiuhalisia, mtoto wa miaka 14 hawezi kujua maana ya ndoa, wajibu katika ndoa na changamoto zake, hivyo kumruhusu aolewe ni uamuzi ambao hauna busara na ndoa hiyo haiwezi kudumu, bali mtoto wa kike ataishia kukosa haki zake za msingi, ikiwamo elimu na kupata mimba katika umri mdogo.
Sisi tunaamini kuwa dawa pekee ya kumaliza ndoa na mimba za utotoni ni jamii nzima kupaza sauti kuzishinikiza mamlaka husika za serikali kuifanyia marekebisho sheria hiyo, ambalo kimsingi imepitwa na wakati katika mazingira ya sasa.
Jambo la kushangaza ni kwamba licha ya makundi ya wanaharakati kupaza sauti wakitaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho ili kuzuia mtoto wa kike chini ya miaka 18 asiruhusiwe kuolewa, serikali haijasikia kilio hicho wala kuonyesha utashi.
Tunasema hivyo kutokana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusema kuwa atakata rufani kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka huu katika kesi iliyofunguliwa na mwanaharakati mmoja kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho.
Katika uamuzi huo, Mahakama Kuu ilikubaliana na ombi hilo na kuielekeza serikali kufanya marekebisho ya kifungu cha umri wa kuolewa uwe kuanzia miaka 18 na kuendelea.
Tunatoa wito kwa serikali kusikia kilio hicho na kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1991 ili kuweka umri wa mtoto wa kike kuolewa unaokubalika.
Kwa kufanya hivyo, tatizo la ndoa na mimba za utotoni litakuwa limepatiwa ufumbuzi sambamba na kuwapa watoto wa kike fursa za kupata elimu. Ni matumaini yetu kuwa wanaharakati kama Tamwa wataendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu athari za ndoa na mimba za utotoni.
Aidha, tunaishauri Serikali kujikita zaidi katika kupiga vita utamaduni wa ulipaji mahari ambao baadhi ya jamii zimeugeuza kuwa biashara kama njia ya kukomesha ndoa za utotoni.










