Maagizo ya waziri kwa TANESCO yasimamiwe

28Apr 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maagizo ya waziri kwa TANESCO yasimamiwe

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amewataka mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme ili kufikia vijiji vyote mwaka 2022.

Alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, akisema kama kuna watumishi wanaoona hawataweza kukamilisha kazi hiyo kujiondoa wenyewe kabla ya kuchukuliwa hatua.

Waziri huyo alipiga marufuku mgawo wa umeme na ukataji wa umeme bila kutoa taarifa kwa wananchi na kwamba kuanzia sasa ambaye hatatoa taarifa atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Maagizo yote mawili yamekuja katika wakati mwafaka kwa kuwa siku za hivi karibuni mgawo wa umeme ulianza na hakukuwa na taarifa, kiasi cha maeneo mengi nchini kukosa nishati hiyo.

Ilianza kwa mitaa michache au umeme kukatika na kurudi kwenye nyumba chache, huku nyingi zikiachwa bila nishati hiyo kwa muda mrefu, na mbaya zaidi hakuna taarifa kwa wananchi jambo lililowafanya wengi kuathirika.

Matumizi ya majenereta yalirejea na hakukuwa na taarifa za mara kwa mara la suala hilo, huku wataalam waliojitokeza walidai kuna hitilafu ya umeme, lakini kwanini hawakutoa taarifa kwa umma ili kuwe na maandalizi hakukuwa na jibu.

Ni muhimu sana kwa TANESCO ambalo ndilo shirika pekee la kuzalisha na kusambaza nishati hiyo likaimarisha kitengo chake cha mawasiliano kuanzia ngazi ya wilaya na kutumia vyema mitandao ya kijamii katika kusambaza taarifa hizo, kuliko kusubiri taarifa zote kutolewa makao makuu.

Miaka miwili nyuma lilikuwa ndilo shirika pekee linalotoa taarifa kwa umma mara kwa mara kupitia mitandao ya kijamii ambazo zilisambaa haraka, lakini utaratibu huo ulisitishwa na hadi sasa kasi ya kutoa taarifa imepungua, jambo ambalo tunaona bado linatakiwa kufanyiwa kazi ili kurudisha utaratibu wa utoaji taarifa kwa umma.

Jingine ni kuunganisha umeme, bado kuna wananchi wengi wa mjini na vijijini wameshapeleka maombi ya kuunganishiwa umeme, lakini hadi sasa hawajapata huduma hiyo.

Sababu kubwa inayotolewa ni vifaa au danadana nyingine ambazo hazina sababu, huku wanaoumia zaidi ni wale ambao kuunganishwa kwao kunahitaji nguzo kwa kuwa hilo eneo hakua miundombinu kabisa.

Ni muhimu sana TANESCO ikatekeleza kwa kasi uunganishaji wa umeme, kwa kuwa wakati mwingine inashangaza iweje watu wa mjini ambako kuna miundombinu wanaomba kuuganishiwa nishati hiyo.

Kubwa zaidi ni kukatika kwa umeme bila taarifa ambako kumaathiri wengi kwa mali zao kuharibika, kushindwa kufanyakazi hasa wale ambao wanategemea nishati hiyo na hawana majenereta.

Nishati ya umeme ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi, ni muhimu sana ikapatikana kila wakati, vinginevyo ni kukwamisha. Kama kuna matatizo ya msingi, ni vyema yakafanyiwa kazi ipasavyo ili wananchi wapate umeme kila wakati.

Tunaona kwamba maagizo ya Waziri Kalemani kwa TANESCO utekelezaji wake unawezekana kabisa, isipokuwa kinachoweza kuukwamisha ni usimamizi wake.

Maagizo haya si mapya kutolewa na waziri hiyo kwa mameneja wa mikoa, lakini haijulikani ni sababu zipi zimesababisha yasitekelezeke. Aliwahi kusema kuwa kama umeme utakatika kwenye maeneo yao bila sababu maalum watawajibishwa.

Tinashauri kwamba usimamizi wa maagizo hayo uwepo, kwa kuwa watendaji wengi wa shirika hilo wamekuwa wakifaqya kazi kwa mazoea. Bila hivyo, kero kwa watumiaji wa umeme hazitaisha.