Ligi Kuu ya Wanawake isifanywe kama Taifa Cup

01Jun 2016
Mhariri
Lete Raha
Ligi Kuu ya Wanawake isifanywe kama Taifa Cup

HATIMAYE kwa mara ya kwanza katika historia ya soka ya Tanzania, msimu ujao kutakuwa na Ligi Kuu ya wanawake.

Hiyo inafuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wiki iliyopita kuingia Mkataba wenye thamani ya Sh. Bilioni 1 na kampuni ya Azam Media Limited kwa ajili ya michuano hiyo.

Azam TV imenunua haki za matangazi ya moja kwa moja ya Televisheni na TFF kwa ajili ya Ligi Kuu ya Wanawake na pia Ligi Kuu ya Vijana wa umri chini ya miaka 20, ambako kila eneo wametoa Sh. Bilioni 1 kwa miaka mitano.

Zoezi hilo lilifanyika Ofisi za makao Makuu ya Azam Media Ltd eneo la TAZARA, Dar es Salaam upande wa TFF ukiwakilishwa na Rais wake, Jamal Malinzi na Azam Media wakiwakilishwa na Mtendaji wake Mkuu, Muingereza Rhys Torrington.

Katika hafla hiyo fupi, Torrington alisema Mkataba huo ni wa miaka mitano na lengo lao ni kuendelea kusaidia kuinua michezo Tanzania, wakati Malinzi alisema kwamba Ligi Kuu ya Wanawake itaanza kwa kushirikisha klabu 10 Agosti mwaka huu na Ligi ya U20 itashirikisha klabu zote za Ligi Kuu ya Wanaume.

Malinzi alisema Ligi ya Wanawake itaanza na timu 10 baada ya hapo Chama Cha Soka ya Wanawake (TWFA) kitatengeneza muundo wa timu kupanda na kushuka.

Kama tulivyosema, kwa mara ya kwanza tutakuwa na Ligi Kuu ya wanawake – maana yake hatukuwahi kuwa na Ligi Kuu ya akina mama Tanzania, je hizo timu zinazokwenda kushiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza zimetoka wapi na zimepatikana vipi?

Tunachoona hapa TFF na TWFA wanatafuta njia nyepesi ya kupata timu za kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake, jambo ambalo si zuri na litafanya pia tusiwe na mwanzo mzuri katika ligi hiyo.

Lete Raha kwa uzoefu wetu tunapenda kuwashauri TFF, kwanza waendeshe ligi maalum ya kuwania kufuzu Ligi Kuu ya Wanawake, badala ya kuteua kabisa timu 10 za kuanzisha ligi hiyo.

Ligi Kuu ya Wanawake isifanywe kama Kombe la Taifa kwa kuteua timu kutoka mikoa tofauti zishiriki – hapana, bali timu zishindanishwe kuwania kucheza ligi hiyo kwa kushiriki ligi maalum ya mchujo wa kuwania kucheza Ligi Kuu ya Wanawake msimu ujao.

Kama TFF inataka kuleta kitu bora, basi isitafute njia ya mkato – bali itumie taratibu nzuri ambazo mwishowe zitatupatia timu bora zenye wachezaji bora zitakazotengeneza Ligi Bora ya Wanawake Tanzania. Lete Raha tunawasilisha maoni yetu.