Licha ya uchaguzi wa nafasi nyingine, lakini macho ya wengi yapo kwenye nafasi ya rais, ambayo ina wagombea watano, baadhi wametumia vyema mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kueleza kwanini wanagombea nafasi hiyo kubwa katika chambo hicho.
Sheria iliyoanzisha TLS imeeleza malengo tisa ambayo ni kudumisha na kuboresha viwango vya mwenendo wa taaluma ya sheria nchini, kusaidia upatikanaji walimu ya sheria kwa wanasheria.
Mengine ni kusaidia serikali na mahakama kwenye mambo yanayohusu sheria na utungaji wake, na hii ndio inaifanya TLS mdau mkubwa wa kutoa maoni kuhusu maboresho au utungaji wa sheria.
Aidha, lengo jingine ni kuwawakilisha na kuwalinda mawakili na watu wa kwenye taaluma ya sheria kwenye utekelezaji wa sheria nchini.
Pia, inasaidia jamii kwa kuipa elimu na msaada wa kisheria pale inapohitaji.
Yapo mengi ya msingi ambayo TLS ina wajibu wa kuyasimamia ipasavyo na kuwa kiungo muhimu baina yake na serikali, mawakili na jamii, ili kufikia malengo ya haki kwa wanajamii wote.
Matarajio ya jamii ni kuwa wanachama wa TLS wataleta mgombea sahihi ambaye ataendana na mazingira sahihi ya shughuli za sheria na mawakili nchini.
Wanachama wa TLS ndio wanajua kati ya wagombea wote nani atafaa na atakuwa mgombea sahihi kwa sifa za kitaaluma, uzoefu na uelewa mkubwa wa masuala ya sheria, mifumo na jamii ambayo ni mnufaika.
Tunatambua kuwa TLS kwa kushirikiana na mahakama inatoa msaada wa kisheria kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kuajiri wakala katika mahakama ambazo ni lazima mshtakiwa au mlalamikaji awakilishwe na wakili.
Wapo mamia ya wananchi wanakosa msaada wa sheria kiasi cha haki za msingi kupotea, na ni muhimu sana huduma hii ikapanuliwa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa haraka zaidi.
Ni muhimu kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa huduma hiyo hasa maeneo ya vijijini ambayo miundombinu yake bado ni changamoto, na mwananchi anasafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Wapo waliofungwa siyo kwa sababu walistahili, lakini kwa kuwa walikosa huduma ya uwakili au msaada wa sheria tangu mwanzo wa shauri lake.
Tunatambua kazi inayofanyika ikiwamo kuwatembelea wafungwa katika Magereza mbalimbali na kutoa msaada wa kisheria kwao, lakini bado kuna uhitaji mkubwa kulingana na mashauri yaliyopo au ukandamizaji haki unaojitokeza.
Pia, tunarajia wataleta mgombea ambaye atasisitiza umuhimu wa kuifikia jamii kutoa elimu ya uelewa wa masuala mbalimbali ya sheria, ili wasiingie kwenye tatizo ni kwa kutoelewa sheria.
Tunawatakia uchaguzi mwema TLS na ni matarajiao ya jamii watachagua kiongozi sahihi kwa wakati sahihi, kwa kuhakikisha anayepatikana ataifikisha katika malengo yake ikiwamo ubunifu wa kuifikia jamii.
Mawakili wana changamoto zao na wanapochagua kiongozi wanatarajia alete mabadiliko makubwa, ili sehemu kubwa ya changamoto zitatuliwe, ikiwamo kuisaidia jamii kwa kiasi kikubwa.
Tunajua haki ya kila mtu imetajwa katika katiba ya nchi, na mchakato wa kutoa haki unahusisha vyombo vingi, lakini kwa msaada wa wakili haki stahiki ya mtu itapatikana kwa wakati katika muhimili wa utoaji haki.
Kilio cha kuminywa kwa haki ni kikubwa na hasa katika mihimili ambayo ni lazima wanasheria hususan mawakili wanatakiwa kuwatetea wananchi, na ndiyo umuhimu wake katika kutekeleza malengo yake ya msingi unaoonekana.










