Kamati Bunge iharakishe mgogoro wa Naibu Spika

05Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kamati Bunge iharakishe mgogoro wa Naibu Spika

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilisusia kushiriki vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kwa juma moja lililopita ikipinga uendeshaji wa msaidizi huyo wa mkuu wa mhimili huo wa dola.

Juzi wabunge wa upinzani walitoka tena ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya kiongozi huyo kuingia, ikiwa ni siku ya nne mfululizo kufanya hivyo dhidi ya Naibu Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani wa serikali.

Jumatatu, uongozi wa kambi hiyo ulitangaza kutokuwa na imani na Naibu Spika huyo na uliwasilisha kwa uongozi wa Bunge Jumatano hoja ya kumng'oa yenye sababu sita.

Uendeshaji wa Bunge wa Naibu Spika, tunaamini Nipashe, ni kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Bunge kama ilivyo hoja ya kutokuwa na imani na uongozi wa Dk. Ackson.

Kambi hiyo sasa inasubiri uamuzi wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili iwasilishe bungeni kwa ajili ya mjadala.

Na muda huo wa kusubiri, tunaona Nipashe, ndiyo unaweza kuathiri kabisa mwenendo wa mkutano wa tatu wa Bunge la 11.

Ikumbukwe kuwa mkutano unaondelea Dodoma sasa ni muhimu zaidi miongoni mwa vikao vya mwanzoni vya mwaka wa kwanza wa Bunge jipya kwa sababu unajadili misingi ya uendeshaji wa nchi kwa miezi 12 ijayo, kuanzia Julai 1.

Mkutano wa bajeti, tunaona Nipashe, utakuwa na manuufaa pale tu ambapo mipango ya serikali katika wizara mbalimbali itapata si tu mkakati mbadala kutoka hotuba za makadirio ya bajeti za Mawaziri vivuli, bali pia mchango wa wabunge hao katika kurekebisha mikakati iliyowasilishwa na Mawaziri wa serikali.

Kutokana na mfumo wa uongozi wa nchi kisiasa kuegemea kwenye uanachama wa vyama vya siasa, tunafahamu Nipashe, mawazo ya serikali, mara nyingi, hupitishwa kama yalivyo na wabunge wa chama tawala wanapoketi kama kamati.

Kwa sababu bajeti za wizara zilizojadiliwa wiki iliyopita hazikuwa na michango mbadala kwa nia ya kuboresha, na kwa sababu Jumatano ndiyo kilele cha maana halisi ya kuwapo kwa Bunge la Bajeti, tuchukue fursa hii, basi, Nipashe,
kuiomba Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuipa uzito wa kipekee hoja ya wapinzani iliyo mbele yake ili iwe imepatiwa ufumbuzi ifikapo mwisho wa shughuli za Bunge kesho Jumatatu.

Aidha, wakati sakata la kupingwa kwa Naibu Spika likiendela kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, tunaunga mkono pia, Nipashe, maoni ya Mwenyekiti wa wabunge wa CCM mkoa wa Mwanza, Richard Ndassa ya juzi.

Ndassa, ambaye pia ni Mbunge wa Sumve, aliliambia gazeti hili kuwa kuna haja Kiongozi Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni ambaye ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya mazungumzo ya kuridhiana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Ndassa alishauri kufanyike maridhiano kati ya serikali na upinzani ili shughuli za Bunge ziendelee kukiwa na ushiriki wa pande zote mbili.