Habari nzuri kwa Watanzania ni kwamba nahodha wa timu yetu ya Taifa 'Taifa Stars', Mbwana Samatta ni kati ya wachezaji 30 walioingizwa kwenye orodha ya awali ya kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika.
Samatta anayechezea KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji, ameingia na wachezaji wawili wa Afrika Mashariki, kipa Mganda Dennis Onyango, anayechezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kiungo Mkenya, Victor Wanyama anayechezea Tottenham Hotspur ya England.
Orodha hiyo inaongozwa na Waalgeria watatu, mshambuliaji wa mabingwa wa England, Riyad Mahrez, Islam Slimani wa Leicester City na El Arabi Hillel Soudani wa Dinamo Zagreb.
Mkongwe Samuel Eto’o anayechezea Antalyaspor ya Uturuki naye yumo kwenye orodha, pamoja na Mcameroon mwenzake, Benjamin Mounkandjo wa Lorient.
Wengine ni Serge Aurier (Ivory Coast na PSG), Eric Bailly (Ivory Coast na Manchester City), Yao Kouasi Gervais ‘Gervinho’ (Ivory Coast na Hebei Fortune), Mohamed Salah (Misri na Roma), Mohamed El Neny (Misri na Arsenal).
Wamo pia Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon na Dortmund), Andre Ayew (Ghana na West Ham), William Jebor (Liberia na Wydad Athletic Club), Mehdi Benatia (Morocco na Juventus), Hakim Ziyech (Morocco na Ajax), John Mikel Obi (Nigeria na Chelsea), Kelechi Iheanacho (Nigeria na Manchester City).
Wengine ni Ahmed Musa (Nigeria na Leicester City), Cedric Bakambu (DR Congo na Villareal), Yannick Bolasie (DRC na Everton), Sadio Mane (Senegal na Liverpool), Kalidou Koulibaly (Senegal na Napoli), Keegan Dolly (Afrika Kusini na Mamelodi Sundowns), Itumeleng Khune (Afrika Kusini na Kaizer Chiefs, Aymen Abdennour wa Tunisia na Valencia, Wahbi Khazri (Tunisia na Sunderland) na Khama Billiat (Zimbabwe na Mamelodi Sundowns).
Hii ni nafasi nyingine nzuri kwa mchezaji huyo kuingia tu kwenye orodha ya awali kuwania tuzo hiyo, itakayotolewa Januari 5, mwakani, baada ya mwaka huu kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
Samatta alishinda tuzo hiyo akiweka rekodi ya mchezaji wa kwanza wa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla kuwa Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika baada ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na klabu ya TP Mazembe ya DRC mwaka jana na kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.
Ni mafanikio hayo yaliyomfanya anunuliwe na klabu ya Genk alipokwenda kumalizia msimu uliopita na kuisaidia kupata tiketi ya kucheza michuano ya Europa League mwaka huu. Na tayari Samatta ameiwezesha Genk kufika hatua ya makundi ya Europa League baada ya kuvuka vizingiti vyote vya hatua za awali za mchujo.
Wakati Watanzania tukizidi kufurahia mafanikio ya Samatta, tunapata sababu nyingine ya kuendelea kumfurahia nyota wetu huyo kufuatia uteuzi huu wa CAF.
Tunaamini ni uwezo wake umeifanya CAF imwingize katika orodha hiyo ya awali ya wachezaji wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika akitoka kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora anayecheza Afrika.
Sisi Nipashe la zaidi hatuna, isipokuwa kumpongeza kwa uteuzi huo na kumtakia kila la heri katika safari yake kuelekea kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika.










