Hongera Edward Christopher kufunguka ukweli wa mambo

07Feb 2016
Mhariri
Lete Raha
Hongera Edward Christopher kufunguka ukweli wa mambo

MCHEZAJI wa zamani wa Simba, Edward Christopher 'Edo', alikuwa ni tumaini jipya la taifa katika medani ya soka.
Akiwa na umri mdogo, Edo alitisha kila alipoingia uwanjani na kufunga magoli.

Mashabiki wa mchezo huo unaoongoza kwa kupendwa duniani walitabiri makubwa kwa straika huyo.
Walikuwa wakimuona Mbwana Samatta mpya anaibukia na kwa kuwa alipita njia ileile ya Samatta -- kuichezea Simba -- wengi walikuwa wakimuona Edo siku moja akicheza katika ngazi ya juu Afrika na hata Ulaya.
Lakini katika mshangao wa wengi, Edo alitoweka, akaishia kutemwa na sasa anaitumikia Toto Africans ya Mwanza.
Kama ilivyo kawaida ya mashabiki, tuhuma zikabaki kwa klabu ya Simba kwamba imeua kipaji chake na kisha kumtupa, ikiwa ni mwendelezo wa tuhuma dhidi ya klabu kubwa nchini ikiwamo Yanga.
Tofauti na mitazamo hiyo ambayo ni matokeo ya 'mbegu mbaya' iliyopandikizwa, ikaota na kukomaa kwa miaka mingi mawazoni mwa mashabiki walio wengi kwamba klabu hizo huua vipaji vya wachezaji na kuwatupa, Edo amefunguka ukweli.
Mchezaji huyo mwenye kipaji, amebainisha kuwa kushuka kwa kiwango chake hadi kupoteza nafasi yake kulikuwa ni kuendekeza starehe wakati akiwa Simba.
Edo amekaririwa na LeteRAHA katika habari iliyochapishwa kwenye ukurasa wa 3, akisema: "Nimejutia makosa yangu na hiyo imebakia kama historia kwangu kwani nilikuwa napenda sana kujirusha, hivyo nilikuwa nakosa muda wa kutuliza akili na kuufanya mwili wangu uwe tayari kwa kazi kutokana na kuuchosha kwa mambo mengi." Mwisho wa nukuu.
LeteRAHA kwanza inachukua fursa hii kumpa pongezi Edo kwa kuamua kuzungumza ukweli ambao hakika umewashinda wengi waliotangulia.
Wengi kati ya waliotangulia kabla yake kupita katika klabu hiyo na pia Yanga, wamekuwa wakizituhumu klabu hizo kuua vipaji vya wachezaji.
Lakini je, ni kweli kwamba Simba na Yanga hazitaki wachezaji bora kabisa katika timu zao hadi kuua vipaji vyao?
Hawa kina Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa waliojiunga na timu hizi wakiwa wadogo waliuliwa vipaji vyao?
Mchezaji mzuri si lazima atambe katika kila timu aendayo na hilo linatokana na mifumo ya kocha na sababu nyingine zikiwamo nidhamu binafsi kama alivyofunguka Edo.
Hivyo si sawa kwa kila mchezaji anayeshindwa kung'aa Simba au Yanga kuzituhumu timu hizo kuua vipaji na kujaribu kuficha mengineyo ya kiufundi ambayo yamechangia kushindwa kutamba kwake.
Mficha maradhi umauti humuumbua. Mchezaji kukataa kuukubali ukweli wa mambo ya kiufundi yanayofanya kiwango chake kishindwe kukua, kamwe hakuwezi kumsaidia kuzifikia ndoto zake. Usitafute kichaka cha kujifichia.