Aidha, viongozi wakuu wa serikali wamesema hakuna marufuku yoyote ya kuvaa barakoa, lakini msisitizo mkubwa ni tahadhari na kumwomba Mungu kwa bidii na ndiyo maana Rais John Magufuli alitangaza maombi ya siku tatu kwa waumini wa dini zote.
Tahadhari hizi zimesisitizwa pia ulimwenguni na kuna nchi nyingi zimefungia wananchi wake kutokana na kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Kama ambavyo msisitizo wa sasa wa serikali ni kuwa Tanzania siyo kisiwa kutokana na kupakana na nchi mbalimbali ambazo zote na zimekumbwa na maambukizi.
Maana yake hata nchini tunaweza kupata maambukizi, hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari ya kujikinga kwa nguvu zote kuhakikisha tunakuwa salama muda wote.
Lakini bado tunaendelea kupokea wageni na watalii wanaokuja kwa sababu tofauti tofauti, ambao wanaingia kwa njia nyingi. Hata hivyo, kwa jinsi virusi vya corona vilivyo, mtu anaweza kupata wakati wowote na mahali popote.
Msisitizo ni muhimu, laini bado tunaona kuna jitihada za makusudi zinatakiwa kufanyika kuhakikisha tahadhari inachukuliwa katika vyombo vya usafiri wa umma kama mabasi, daladala na mwendokasi, ambako maisha yaendelea kama kawaida licha ya kuwapo changamoto ya upumuaji.
Kadhalika, katika maeneo ya biashara ule utaratibu wa kuhakikisha kila eneo kuna maji tiririka na sabuni na mtu anawe kabla ya kuingia kununua au kupata huduma yoyote ni muhimu sana.
Pia, katika maeneo ya taasisi za elimu na shule ambazo mwaka jana zilikuwa na mwongozo wa kuchukua tahadhari, tunaona ni muhimu kwa sasa wakatekeleza ili kuendelea kubaki salama.
Tunasema tahadhari ni muhimu sana ili kuendelea kujilinda na corona inayosumbua dunia kwa sasa. Mathalani unapotembelea kituo kikuu cha mabasi Ubungo ambacho kinatumiwa na watu wa mataifa mbalimbali, jambo la kusikitisha hakuna tahadhari yoyote.
Pia, bado hakuna msisitizo katika kuvaa barakoa kwa wasafiri na watoa huduma, jambo ambalo tunaona ni muhimu sana likafanyika kwa kuwa Ubungo ni kituo kinahudumia watu wengi.
Pia ni muhimu viongozi wa serikali za mitaa, vitongoji na ngazi nyinginezo kushirikiana na wataalamu wa afya wakatoa elimu ya uvaaji wa barakoa, ambao wakati mwingine bila kufuata masharti ni rahisi kusambaza virusi.
Tunaamini wananchi wakielimishwa watafuata na kuchukua hatua madhubuti, kama ilivyofanyika kwenye maradhi mengine ambayo yamewahi kuisumbua dunia na nchi kwa ujumla.










