Kocha Simba afurahia stamina

25Jan 2016
Sema Usikike
Kocha Simba afurahia stamina

KAIMU kocha mkuu wa Simba Mganda Jackson Mayanja amesifu wachezai wake kwa kuimarika na kusema ameanza kutibu gonjwa la stamina na pumzi liliulokuwa likiwakabili.
Kocha huyo alisema kuwa alivyochukua kikosi hicho kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wadau, wanachama na mashabiki wa Simba kuwa wachezaji wa timu hiyo hawana pumzi wala stamina na hilo ndilo alianza nalo.

Jackson Mayanja

"Mnaona wenyewe leo, timu imecheza kwa nguvu dakika zote, na hata wakati mpira unamalizika ukikuwa kwenye himaya yetu na tulikuwa bado tunashambulia kutafuta bao," alisema kocha huyo mara baada ya kumalizika kwa pambano kati ya Simba na JKT Ruvu lililofanyika Jumatano iliyopita uwanja wa Taifa na kupata ushindi wa bao 2-0.
Hata hivyo alisema kuwa bado wachezaji wake hawajawa na stamina na pumzi kwa asilimia 100 na kwamba bado anaendelea kulifanyia kazi taratibu.
"Hivi vitu haviji ghafla. tunavitengeneza taratibu, siyo unaweza kupata pumzi na stamina kwa siku moja tu. Na hata hivyo bado wakati unawapa fiziki wachezaji unatakiwa uwape mbinu za kiufundi, kwa hiyo mashabiki inabidi wavute subira kidogo, ingawa vijana wamenifurahisha na lile tatizo linaanza kupungua," alisema.
Mayanja ameichukua Simba mikononi mwa Muingereza Dylan Kerr aliyetimuliwa kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kushindwa kuifanya timu kucheza soka la kuvutia, lakini pia wachezaji wakionekana kuchoka na kukosa pumzi hivyo kushindwa kuhimili vishindo vya dakika 90 za mchezo.