Kizimbani kwa kukutwa na meno ya tembo

28Jan 2016
Nipashe
Kizimbani kwa kukutwa na meno ya tembo

WATU wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka mawili, likiwemo la kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh. billion 1.4.

Meno ya tembo.

Washtakiwa hao ni Robert Mwaipyana (32) na Ramadhani Mnekea (55), wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Charles Anindo aliwasomea mashitaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Respicious Mwijage.

Anindo alidai kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Januari Mosi na Desemba 21, mwaka jana, katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, washtakiwa walikutwa wamekusanya na kuuza nyara za serikali, vipande 161 vya meno ya tembo yenye uzito wa kilo 220.96.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa meno hayo yana thamani ya dola za Marekani 690,000 ( sawa na Sh. bilioni 1.4), mali ya Serikali ya Tanzania.

Ulidai kuwa washtakiwa walikutwa na nyara hizo bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Upande wa Jamhuri ulidaiwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kesi hiyo itatajwa Februari 9, mwaka huu, na washtakiwa walipelekwa mahabusu.