Kesi ya Bulaya yafutwa rasmi

26Jan 2016
Nipashe
Kesi ya Bulaya yafutwa rasmi

MBUNGE wa Bunda Mjini (Chadema), Esther Bulaya, amewashinda wakazi wanne wa jimbo hilo waliofungua kesi ya kupinga ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na kumshinda mpinzani wake, Stephen Wasira, kutoka CCM.

MBUNGE wa Bunda Mjini (Chadema), Esther Bulaya.

Katika kesi hiyo, Bulaya alikuwa akitetewa na mwanasheria maarufu nchini, Tundu Lissu, huku watuma maombi wakitetewa na Constantine Mutalemwa.
Akitoa uamuzi ya ‘kuipiga’ chini kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Gwae, alidai walalamikaji katika kesi hiyo hawana mamlaka kisheria kufungua kesi hiyo wala hakuna sehemu waliyoonyesha kuathirika na uchaguzi huo.
Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 1 ya mwaka 2015, mjibu maombi wa kwanza (Bulaya), alikuwa akishitakiwa na Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagira, ambao walikuwa na mawakili wawili, ni Mutalemwa na Denis Kahangwa.
Aidha, watuma maombi hao walikuwa wakimlalamikia msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ambaye ni mjibu maombi wa pili na mwanasheria mkuu wa serikali, ambao wote walikuwa wakitetewa na wakili Paschal Malongo.
Jaji Gwae alisema malalamiko ya waombaji hao hayakuonyesha walivyoathirika baada ya Bulaya kushinda uchaguzi na ‘kumgaragaza’ Wasira.
Awali ilidaiwa na walalamikaji hao kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, haukuzingatia sheria na taratibu kwa mgombea wa CCM (Wasira), baada ya kuomba kura zihesabiwe upya lakini alikataliwa na wala hakupewa nakala ya matokeo.
Pia walidai idadi ya kura zilizotolewa katika fomu namba 24B, zinatofautiana na idadi ambayo ilitolewa na Tume ya Uchaguzi (Nec) iliyoonyesha idadi ya wapiga kura ni 69,369 wakati idadi ya vituo vya kupigia kura vikitofautiana na ile iliyotolewa na msimamizi wa uchaguzi ya vituo 199 huku vya Nec vikiwa 190.
Wakati uamuzi huo ukitolewa, Bulaya na wakili wake, Lissu hawakuwapo mahakamani hapo.