Kerr: Hii aibu Simba

13Jan 2016
Lete Raha
Kerr: Hii aibu Simba
  • Asema ni aibu kufukuzwa kisa Mapinduzi Cup, Mayanja aanza kazi

KOCHA Dylan Kerr ameponda maamuzi ya uongozi wa Simba ya kumtimua kazi akisema ni aibu kumfukuza mwalimu kisa Kombe la Mapinduzi.

Kocha wa Simba, Dylan Kerr

Uongozi wa Simba jana ulitangaza kumtimua kazi kocha huyo, siku moja tu baada ya kutolewa katika nusu-fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Majira ya saa 3:12 za asubuhi jana, Lete RAHA ilitinga kwenye bandari ya Zanzibar na kukutana na kocha huyo ambaye alikuwa akiondoka visiwani Zanzibar kurudi Dar es Salaam majira ya saa 3:30 asubuhi kwa ajili ya kukutana na viongozi wa klabu hiyo, ambao hatimaye walimtimua kazi na kumuachia majukumu kocha Jackson Mayanja aliyesaini Simba akitokea Coastal.
Mayanja alianza kuiongoza Simba katika mazoezi ya jana jioni akiwa peke yake.
Katika mazungumzo yake, Kerr alisema kuwa anawashangaa Simba kumfukuza kwa vile tu timu yake imetolewa kwenye Kombe la Mapinduzi na akawataka waangalie hali ilivyo kwa kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, ambao pia wametolewa katika nusu-fainali.
Kerr alisema, “Ninalala na kuamka mapema kwa ajili ya Simba, napambana kila uchao ili kuhakikisha ninaipa ushindi timu yangu. Nachukua muda wangu mwingi kuwa na wachezaji na kuwashauri ili tuweze kusonga mbele, lakini natakiwa kuondoka kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi? Hii ni aibu kwa kweli.
“Mbona kocha wa Yanga hajakumbana na changamoto kama hizi ninazopitia wakati wote tulitolewa kwenye nusu-fainali? Mapinduzi siyo ligi, tunahitaji kufikiria mbali na kutazama zaidi mashindano ambayo yalikuwa na tija kwenye kikosi chetu na ndiyo maana nilitoa nafasi kwa wachezaji ambao hawakuwa wamecheza awali.
“Itakuwa ni kichekesho kwangu kutimuliwa kwasababu ya Kombe la Mapinduzi ni kama bonanza kwani timu shiriki si zote za ligi. Mbona kocha wa Yanga hafukuzwi, kwani kazi yake na yangu kwenye Kombe la Mapinduzi ina tofauti gani? Tazama sasa mwenzangu anaendelea na mipango mingine wakati mimi nikiambiwa ninatimuliwa,” alisema Kerr huku akisisitiza kuwa, hata hivyo, hizo ni changamoto za kawaida kwa makocha.

KISA CHA KUFUKUZWA
Kerr alitimuliwa jana kufuatia kikao na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kujadiliana masuala mbalimbali ikiwamo tuhuma mbalimbali zinazomkabili juu ya mwenendo wa timu.
Muingereza huyo alituhumiwa kwa maelezo kwamba ameshindwa kuifanya Simba icheze vizuri na uongozi unaamini kiwango cha timu kimeporomoka kwa kiasi kikubwa kutoka alivyoikuta Julai mwaka jana ilipoachwa na Mserbia, Goran Kopunovic.
Aidha, amekosolewa kwa kutoa ushauri mbaya kwa uongozi uliosababisha kuachwa kwa wachezaji kadhaa wazuri akiwamo Elias Maguli na kumsajili mchezaji Msenegali, Pape N’daw, ambaye kiwango chake kilionekana kuwa chini na hivyo klabu ikamtema Desemba mwaka jana.
Kerr pia ametuhumiwa kwa ukaidi na kutosikiliza ushauri wa watu anaofanya nao kazi. Anatuhumiwa kutokuwa na maelewano mazuri na wasaidizi wake jambo ambalo lililosababisha aliyekuwa kocha msaidizi, Suleiman Matola, na wa mazoezi ya utimamu wa mwili, Mserbia Dusan Momcilovic kuondoka.