Ikungi yashika mkia ujenzi wa maabara

25Jan 2016
Sema Usikike
Ikungi yashika mkia ujenzi wa maabara

WAKATI Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ikishika nafasi ya kwanza mkoani Singida kwa ujenzi wa maabara kwa kujenga vyumba 53 na vingine vitatu vikiwa katika hatua za mwisho kukamilika, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imeshika nafasi ya mwisho (6) baada ya kujenga vyumba vinne tu kati ya mahitaji halisi ya vyumba 90.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Parseko Kone (wa pili kulia) akikagua ujenzi wa maabara ya sekondari wilayani Ikungi

Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Suleman Nkondo, alisema hayo wakati akitoa taarifa kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
Nkondo alisema kuwa, vyumba vingine 45 katika halmashauri ya wilaya ya Ikungi vipo kwenye hatua ya renta, wakati vyumba 37 vipo hatua ya msingi na vinne ujenzi wake bado haujaanza kutekelezwa.
Alifafanua kuwa halmashauri ya Singida imekamilisha vyumba 19, huku vingine 59 vikiwa hatua ya ukamilishaji, wakati Manispaa ya Singida imekamilisha17, huku 34 inamalizia na Manyoni imekamilisha 23 na inamalizia 57, huku vitatu vikiwa kwenye renta.
Kaimu ofisa elimu huyo alisema kuwa hadi sasa mkoa wa Singida umekamilisha ujenzi wa vyumba 120, kati ya mahitaji halisi ya vyumba 413, katika shule zake zote 160 za sekondari.
Mapema Mkuu wa mkoa huo, Dk. Parseko Kone, alitaka kuchukuliwa hatua kali za sheria dhidi ya mwalimu atakayebainika kutoza mchango wa aina yoyote kutoka kwa wazazi au mlezi, kuhusiana na wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu.
Mkuu huyo wa mkoa alitaka pia kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wote watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao kujiunga na kidato cha kwanza kwa kisingizio cha michango, ambayo hata hivyo imefutwa na serikali.
Alisema kuwa anaamini wanafunzi wote 13,383, wakiwamo wasichana 6,959 waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza wataripoti kwenye shule mbalimbali walizopangiwa.