Huduma muhimu zinatakiwa kituo kikuu cha mabasi Ubungo

21Jan 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Huduma muhimu zinatakiwa kituo kikuu cha mabasi Ubungo

KITUO cha Mabasi yaendayo Mikoani na Nchi jirani Ubungo (UBT), kinategemewa na wasafiri wengi jiji la Dar es Salaam na watokao mikoa mbalimbali na nchi jirani.

ABIRIA WAKISUBIRIA USAFIRI KITUO CHA MASI UBUNGO

Kutokana na kukua kwa kasi kwa shughuli mbalimbli za kiuchumi , kielimu na mengineyo katika jiji la Dar es Salaam, usafiri wa mabasi ni muhimu kwa watu wa kada tofauti wakiwamo wafanyabiashara, wanafunzi, wazee, wagonjwa na wengineo.Kila mmoja kwa umuhimu wake.
Hata hivyo, katika kituo cha mabasi Ubungo, hali ni tofauti ya upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo vyoo,.zahanati na mengineyo.
Tofauti na ilivyokuwa hapo awali kabla ya upanuzi wa barabara ya Morogoro walau huduma muhimu kama vile vyoo, eneo la kupumzikia abiria na kufanywa usafi kila siku.
Huduma hizo zilikuwa muhimu kwa abiria na watu wote wakati ule na hata sasa.
Hali ilivyo kwa sasa ni kwamba, hakuna utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa huduma hizo zinapatikana matokeo yake ni kukithiri kwa uchafu hasa majira ya usiku watu hujisaidia hovyo hata kuhatarisha afya za wasafiri, wapitia njia na walizungukao eneo hilo hasa wanaofanya biashara wakiwemo mama lishe.
Katika kituo hicho, mabasi ya abiria zaidi ya 400 huingia na kutoka kila siku.Abiria hutozwa ushuru wa Sh 200. Watu wanaoingia na kutoka hukadiriwa kufikia 10,000 kwenye kituo hicho.
Kwa sasa hali ya kituo hicho ni ya kukatisha tamaa kutokana na halisi ilivyo kiasi kwamba haifahamiki fedha zinazokusanywa kwa nini haziambatani na huduma tarajiwa?.
Kwa kawaida fedha zinazotozwa katika eneo fulani la biashara au huduma hutarajiwa liambatane na uimarishaji wa upatikanaji wa huduma bora katika eneo husika ikiwamo miundombinu yake.
Huduma hizo ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya kupumzika na kuwasitiri wateja wakati wa jua na mvua inaponyesha , eneo la kutupia taka na upatikanaji wa maji safi ya bomba.
Maeneo ya kupumzikia yanaweza kuwa na vyombo vya habari vya kieletroniki kwa ajili ya kutoa taarifa rasmi za mambo ya hapa na pale yanjayohusu eneo hilo ikiwemo abiria kuwatafuta ndugu zao na mengineyo iwapo mtoto au mtu mzima kupotea kutokana na ugeni ama tatizo la kiakili.
Kile ambacho kinaitwa ushuru au tozo la kila abiria anayeingia kituoni hapo, hakiendani na hali halisi ilivyo..
Iwapo mamlaka husika zinaona kituo kinafaa kuendelea kutoa huduma hiyo ni vyema ikazirudisha huduma za awali ili kuwafanya wasafiri kuwa katika eneo salama na si vinginevyo
Hali ya kituo hicho kwa sasa haiwakeri abiria tu hata madereva wanaoanzia na kumalizia shughuli zao za kujitafutia riziki kila siku katika kituo hicho.
Kituo hicho, kinapaswa kuendana na hadhi ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kuwa na huduma muhimu zinazotakiwa kuwa katika kituo chochote cha usafiri wa umma.