Hayo yalisemwa jana mjini Zanzibar na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa ZEC alipokuwa akizungumza na Nipashe.
Nipashe ilitaka kujua msimamo wa tume kuhusu matakwa ya vyama vya siasa vilivyojitoa, kutaka picha na taarifa zao kuondolewa katika karatasi za kupigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa marudio.
Kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha sheria uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984, mgombea hawezi kujiondoa baada ya Tume kukamilisha kazi ya uteuzi wa wagombea ambayo ilifanyika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.
Alisema ZEC iliviandikia vyama kutaka wathibitishe kama wagombea wao wapo hai au kuna waliofariki na sio kutaka kufahamu kama watashiriki uchaguzi wa marudio au hawatashiriki.
“Tume ilifuta matokeo ya uchaguzi na sio mchakato wa wagombea ndiyo maana wagombea wale wale wa urais, uwakilishi na udiwani ndiyo watakaoshiriki uchaguzi wa marudio wa Zanzibar na si wagombea wapya,” alisisitiza Kiongozi huyo.
Alisema kuwa maandalizi yote ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio yamekamilika na kazi moja tu imebakia ya kuchapisha karatasi za wapiga kura kabla ya kufanyika uchaguzi huo Machi 20 mwaka huu.
“Wagombea wote wa nafasi mbali mbali walikula kiapo mahakamani cha kushiriki uchaguzi haiwezekani kujitoa kabla ya kukamilika uchaguzi wenyewe," alisema
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema yeye binafsi aliiandikia barua ZEC akiiarifu kuwa hatashiriki uchaguzi huo hivyo atashangaa iwapo jina lake litajitokeza kwenye uchaguzi huo wa marudio.










