Waziri January amewaeleza wafanyabiashara na wawekezaji wa Italia fursa mbalimbali za biashara zinazopatikana nchini pamoja na mageuzi makubwa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji yanayofanyika chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Alisema mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama na rafiki kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali ili kuhakikisha wafanyabiashara wanatekeleza majukumu yao.
Alisema Tanzania inazingatia misingi ya utawala bora pamoja na kuzungukwa na nchi saba ambazo hazina bandari na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma kwenda katika nchi hizo.
Pia alisema mazingira ya biashara na uwekezaji ya Tanzania ni salama kwa sababu imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda mitaji na uwekezaji wa kigeni pamoja na serikali kutambua sekta binafsi kama injini ya maendeleo kiuchumi.
“Napenda kuwasihi wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Italia kuja kuwekeza Tanzania kwani licha ya kuwa na mzingira salama, pia kuna fursa za kuwekeza katika sekta mbalimbali kama nishati, utalii, kilimo, afya na elimu,” alisema January.
Alisema Tanzania ni mwanachama wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) ambalo linahusisha watu zaidi ya bilioni 1.5, itawezesha wafanyabiashara wa Italia kuwafikia watu hao kupitia soko hilo.
Alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na Italia katika kutekeleza Mpango wa Mattei kwa maslahi ya pande zote mbili na kuwasisitiza kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania na visiwani Zanzibar.
Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Alfredo Cestari, alisema utekelezaji wa mpango wa Mattei utakapoanza utazingatia maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau na miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika ikiwamo Tanzania.
Tanzania ni moja kati ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) na Euro bilioni tano za awali zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.










