Watumishi Mafinga kufikishwa kortini

10Feb 2016
Mafinga, Iringa
Nipashe
Watumishi Mafinga kufikishwa kortini

HALMASHAURI ya Mji wa Mafinga imepanga kuwafikisha Mahakamani watumishi tisa wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi wanaodaiwa kufanya uzembe na kusababisha vifo vya baadhi ya wajawazito.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Shaib Nnunduma, alisema kwa sasa uongozi wa halmashauri hiyo unakamilisha taratibu za kisheria ili kuwafikisha watumishi hao mahakamani, akiwamo mganga mfawidhi, kutokana na uzembe kazini.

Nnunduma alisema watumishi hao kutokana na hali ilivyokuwa tayari wamepumzisha kazi kuanzia Januari 26, mwaka huu, na kulingana na taratibu za utumishi watapewa hati za mashtaka ili waweze kujieleza na taratibu zingine zinafuata.

Hivi karibuni ziliripotiwa taarifa za mama mmoja, Sauda Myinga, alifika hospitalini hapo kujifungua lakini kutokana na uzembe uliofanywa na wahudumu, hakupata huduma hadi alipofariki dunia Januari 11, mwaka huu. Mama huyo alipaswa kupata huduma ya upasuaji baada ya kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jowika Kasunga, amezitaka Halmashauri za Wilaya ya Mufindi na ya Mji wa Mafinga kushirikiana katika kutoa huduma kwa wananchi.