Rai hiyo ilitolewa jana na baadhi ya wazee wastaafu waliojiunga na mfuko huo jijini Dar es Salaam katika mkutano baina yao na mfuko huo.
Mmoja wa wanachama wastaafu wa mfuko huo, Amani Mahenge, alisema kuwa ingawa mfuko unawasaidia kupata matibabu lakini wanapata wakati mgumu kwa kutojua sehemu sahihi ya kupeleka malalamiko yao pindi watakapokwazwa.
“Tunakuwa na wakati mgumu pale tunapopata matatizo huwa hutuna sehemu iliyowekwa ili sisi kupeleka malalamiko yetu yashughulikiwe kwa haraka ,”alisema Mahenge.
Alisema pia wanapokwenda katika baadhi ya hospitali za serikali, wauguzi wengi wamekuwa wakiwadharau na kuwajibu vibaya kwa kuwa tu wana kadi hiyo.
“Wauguzi wengi wakikuona umeshika kadi hiyo hata kama alikuwa ameanza kukuhudumia vizuri basi huduma itabadilika, hivyo basi ni vyema mfuko ukaanzisha dawati hilo haraka ili nasisi tuweze kupeleka matatizo yetu na yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka,”alisema.
Alishauri serikali iweke utaratibu maalum au ivielekeza vituo vya matibabu kutoa kipaumbele cha huduma za matibabu kwa wastaafu, kwani kundi hilo lina wateja wengi ambao hawawezi kupanga mstari na kusubiria huduma ya afya.
Eugin Mkongoti ambaye ni Mkurugenzi wa Mfuko huo, aliwatoa hofu wastaafu hao na kuwaahidi kulifanyia kazi suala lao kwani mfuko unaamini kwamba wazee ni tunu kwa taifa.
”Ni ukweli uliowazi kuwa wastaafu ndiyo waasisi wa mfuko huu, kwa maana ndiyo walianza kuchangia fedha zao ili kupata kadi za bima ya afya katika mazingira ambayo hakuna aliyejua nini kitatokea hapo baadaye,” alisema.
“Wazee hawa walifanya kila kitu kwa imani tu, kwamba siku moja mfuko huu utafaa. Kimsingi walikuwa kama wanacheza kamari, imani yao na matarajio yao kwetu ndiyo yameuwezesha mfuko kufika hapa ilipo hivyo hatuna budi kuwasikiliza na kukamilisha mahitaji yao.”










