Wanawake watatu mbaroni kwa wizi wa simu 61 Shinyanga

20Dec 2023
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Wanawake watatu mbaroni kwa wizi wa simu 61 Shinyanga

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, linawashikilia wanawake watatu ambao ni raia wa Burundi kwa tuhuma za wizi wa simu uliokubuu katika maeneo mbalimbali ya minada, pamoja na wanaume ambao hulala nao kufanya biashara ya ngono.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi akionyesha Simu 61 ambazo wamezikamata kutoka kwa Wanawake 3 ambao ni Raia wa Burundi.

Wanawake hao ambao majina yao yamehifadhiwa, wamekuwa wakiiba simu hizo katika minada ya Buhongwa Jijini Mwanza, Kahama pamoja na Minada ya Shinyanga.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkaani Shinyanga, Janeth Magomi, amebainisha hayo leo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, kufuatia masako ambao wameufanya kwa kipindi cha kuanzia Novemba hadi Desemba 19 mwaka huu.

Amesema wanawake hao wameingia hapa nchini kinyume na utaratibu kama wahamiaji haramu, na wamefanikiwa kuwakamata wakiwa na simu 61 ambazo huziiba kwenye minada mbalimbali mkoani Mwanza na Shinyanga na kisha kuzipeleka kwao Burudi kwa ajili ya kuziuza.

“Jeshi la Polisi tunashirikiana na Uhamiaji sababu wanawake hawa wameingia hapa nchini kama wahamiaji haramu kwa ajili ya kufanya wizi huo wa simu kwenye minada, pamoja na wanaume ambao hulala nao, na tayari tumeshamkamata pia kiongozi wao ambaye yupo huko Burundi,” amesema Magomi.

Katika hatua nyingine Kamanda, ametaja vitu vya wizi ambavyo wamevikamata, kuwa ni mafuta ya dizeli lita 260 yaliyokamatwa kwenye mradi wa SGR, pikipiki 7, Tv 4, vyuma vya kuchimba visima 9, goroli za karasha 106, pombe ya moshi lita 173, subwaoofa 2, na noti bandia 9.

Ametaja vitu vingine kuwa ni mabomba 11 ya kunyonya mafuta, baiskeli 1, vipande vya nondo 6, spika 2, bangi misokoto 15, vifaa vya kupia ramli chonganishi ambayo ni mikia ya 8 idhaniwayo kuwa ni ya mnyama aina ya nyumbu, na simba, pamoja difu ya gari aina ya Toyota.

Aidha, amesema Jeshi hilo katika kudhibiti ajali za usalama barabarani, wamefanikiwa kukamata jumla ya makosa mbalimbali 2,806 yakiwamo matano ya kusababisha ajali, na mingine ni mwendokasi, na kutoa wito kwa madereva katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, watii sheria za usalama barabarani.

Kamanda pia ametaja mafanikio ambayo wameyapata kupitia kesi za mahakamani, kuwa kesi moja ya kuharibu mali mtuhumiwa alifungwa jela miezi mitano, kesi mbili za pikipiki washitakiwa walihukumiwa kwenda jela miaka miwili hadi mitatu na kesi ya kubaka mtuhumiwa alifungwa miaka 30.