Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Katibu Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni CCM, Solomon Itunda, alisema wanachama waliochukua fomu hadi pazia linafungwa ni 71.
Alisema kwa siku ya jana wanachama watano walichukua fomu na kufunga idadi hiyo ya wanachama waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.
“Leo (jana) hii tumepokea wanachama watano ambao wamejitokeza katika vituo vyetu vya Dodoma na Dar es Salaam kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hii ya Uspika iliyoachwa wazi,” alisema Itunda.
Itunda alisema kwa siku ya jana katika kituo cha Dodoma ni mwanachama mmoja ndiye aliyejitokeza kuchukua fomu wakati katika Ofisi ya Lumumba jijini Dar es Salaam ni wanachama wanne na Afisi Kuu ya Zanzibar hakuna mwanachama aliyejitokeza kuchukua.
Itunda, alimtaja aliyechukua fomu Ofisi Kuu ya CCM Dodoma kuwa ni Samwel Magero.
“Ofisi ndogo ya Lumumba waliochukua fomu ni Rahimuddin Ismail, Alex Mwita, Themistocles Laurian Rwegasira pamoja na Grangay Nyalohala,” alisema Itunda.
Alisema kukamilika kwa kazi hiyo ya kuchukua fomu iliyoanza Januari 10, mwaka huu kunatoa nafasi kwa vikao vingine kuanza.
“Baada ya kuchukua na kurejesha fomu, sasa hatua inayofuata ni vikao vingine kuketi ili kuanza kufanya mchujo wa kupitisha jina moja litakalo kiwakilisha chama katika kugombania nafasi hii ya Uspika,” alisema Itunda.
Alisema pamoja na wanachama hao 71 kuchukua fomu lakini kati yao wawili wameshindwa kurejesha.
Aidha, alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha demokrasia ndani ya chama hicho.
“Lakini pia ninawashukuru wanachama wote ambao wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama,” alisema.










