Wananchi watumia maji machafu, Mkandarasi atelekeza mradi

23Jul 2023
Marco Maduhu
KAHAMA
Nipashe Jumapili
Wananchi watumia maji machafu, Mkandarasi atelekeza mradi

WANANCHI wa kijiji cha Mwaningi Kata ya Bulige Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, wamelalamika kuendelea kutumia maji machafu ya kwenye mabwawa na kuhatarisha afya, huku makandarasi ambaye anatekeleza mradi wa maji kijijini humo amedaiwa kuutelekeza.

Modesta Masai mkazi wa kijiji cha Mwaningi Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama akitoka kichota maji katika bwawa maji ambayo siyo salama kwa matumizi ya binadamu.

Wamebainisha hayo kwenye ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja, alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi.

Mmoja wa wananchi hao Martha Charles, amesema kijiji hicho kina kabiliwa na uhaba mkubwa wa majisafi na salama, na wamekuwa wakitumia maji ya kwenye mabwawa kwa matumizi yote ya nyumbani ikiwamo na kunywa, na kuiomba serikali iwakamilishie mradi huo wa maji kijijini humo, ili wasitumie tena maji machafu.

“Hapa kijijini hatuna maji salama tunatumia maji machafu ya kwenye mabwawa likiwamo bwawa lilepale, na maji ya kunywa hua tunaweka dawa ya kusafisha maji (shabu) angalau yavutie hata kuyanywa tuna shida kweli ya maji,” amesema Martha.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cypriani Luhemeja, ameagiza mkandarasi ambaye ametekeleza mradi wa maji kutoka kampuni ya Pet Cooperation Limited, kwamba hadi kufikia kesho (Jumatatu), awe amesha ripoti kwa mkuu wa wilaya ya kahama, pamoja na kurudisha pesa za serikali ambazo alikwisha chukua kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

“Muongozo wa Wizara unasema makampuni ambayo yanashindwa kufanya kazi yafutwe kabisa nah ii kampuni ni moja wapo liwekwe kwenye (Black List) sababu lengo kuu la Serikali kutumia Wakandarasi kutekeleza haraka miradi hii ya maji ikamilike haraka, lakini huyo ameleta dharau,” amesema Mhandisi Luhemeja.

Aidha, amemuagiza Meneja Wakala wa Maji Safi na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela, kwamba pesa ambazo atazirudisha Mkandarasi huyo wapewe wananchi wa kijijini humo na kuanza kuchimba Mitaro ya Mabomba, na Mradi huo utekelezwe kwa Force Account na ukamilike Oktoba mwaka huu.

Kwa upande wake Meneja huyo wa Ruwasa, amesema Mradi huo wa Maji ulianza kutekelezwa mwaka jana mwezi Februari na ulikuwa ukamilike June mwaka huu kwa gharama ya Sh.bilioni 2.2, lakini Mkandarasi ameutelekeza huku akiwa ameshachukua baadhi ya fedha, na wakimtafuta wakae wazungumza hapatikani.