Hayo yamezungumzwa kwenye kikao cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga na wadau kutoka katika taasisi mbalimbali ambacho kililenga kufanya tathmini ya vitendo vya ukatili kilichoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa ufadhili wa Shirika la Women Fund Tanzania (WFT) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Kituo cha Polisi Mkoa wa Shinyanga SP. Grace Salia, wazazi wanatakiwa kuendelea kuwasimamia watoto na kuwapatia haki zao za msingi ili kukua katika maadili mazuri.
SP Salia amesema mzazi au mlezi anayeishi na mtoto akishindwa kumpeleka shule na kusimamia malezi ya yake sheria inasema mtu huyo anafungwa miaka mitano au anatoa faini ya milioni 10 au vyote kwa pamoja.
Katika kikao hicho Wakili wa Serikali Mkoa wa Shinyanga Immaculata Mapunda, ametaja sheria na mazingira ya mtoto kufanya kazi ambapo amesema mtoto anaruhusiwa kufanyakazi masaa yasiyozidi sita.
“Sheria ya mtoto inakataza mtoto kufanyakazi zozote ambazo zitamlazimisha mtoto kuingia katika shifti za usiku lakini pia katika mazingira ambayo ni hatarishi mfano kazi za uvuvi, kwenda kwenye bahari, kazi za kwenye madini, kubeba vitu vizito pamoja na kufanyakazi katika mazingira ya kemikali”.
“Basi sisi kama wadau inapoonekana katika mazingira hayo hayajaendana kutokana na matakwa ya kisheria tunaruhusiwa kuwafungulia hao watu mashitaka na kuripoti katika sehemu husika”.










