Wananchi 7,388 vijiji tisa Njombe kunufaika na miradi wa maji

05Mar 2023
Elizabeth John
NJOMBE
Nipashe Jumapili
Wananchi 7,388 vijiji tisa Njombe kunufaika na miradi wa maji

Wananchi 7,388 wa vijiji tisa mkoani Njombe wanatarajia kunufaika na utekelezaji wa miradi mitano ya maji yenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni mbili.

Akizungumza wakati wa zoezi la utiaji saini wa mikataba hiyo,Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Njombe, Mhandisi Sadiki Chaka,amesema miradi hiyo inatarajiwa kutekelezwa kipindi kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja.

Amesema kuwa utiaji saini huo ni kati ya RUWASA mkoa pamoja na mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira za halmashauri za mji wa Njombe,wilaya ya Wanging’ombe na Ludewa pamoja na wakandarasi.

Chaka amesema kati ya miradi hiyo mradi mmoja ni wa ukarabati wa mtandao wa maji wa Wangiwasa na ujenzi wa bwawa la maji taka katika kijiji cha Ngalanga Halmashauri ya Mji wa Njombe.

"Miradi hiyo inatarajia kunufaisha wananchi wapatao 7,388 waishio vijijini na pia wakazi wa mji wa Njombe kupata huduma ya kuboreshewa au kuondoshewa maji taka pamoja na miundombindu mingine vituo 22 vya kuchotea maji vitajengwa"amesema Chaka.

Akizungumza mara baada ya zoezi la utiaji saini,Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka amewataka wakandarasi kuacha ubabaishaji wakati wa kutekeleza miradi hiyo.

"Dhamira Mh. Rais anapotoa hizi fedha za miradi uwa anamaneno anasindikiza anasema angetamani kuona nchi ichemke,sasa nchi kuchemka ni kwamba anatoa kazi anatoa fedha nyinyi mnapata kazi watanzania wenzetu sasa badala nchi kuchemka nyinyi mnaichemsha,mnachukua fedha mradi wa Wanging'ombe una madeni yako Lindi unaacha kazi ya Wanging'ombe unaenda Lindi,Wanging'ombe wanafanya kazi ya kukudai na kwenye simu hupatikani.Tungetamani mmeanza kazi kwetu tufike mwisho kwenye kukabidhiana kazi usikabidhiane kesi"amesema Mtaka.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga,amesema wakati wanaingia madarakani kilio kikubwa cha wananchi ilikua ni upatikanaji wa maji safi.

"Ukienda kule Manda kuna ngoma wanacheza wanakuletea maji machafu kwenye kopo kama hili wanakwambia mh mbunge kunywa maji haya kama na wewe unaweza yamechanganyika na kinyesi cha ng'ombe ilikuwa hali ni mbaya sana lakini tushukuru ndani ya muda mfupi serikali imefanya miujiza"amesema Kamonga.