Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAMSTOA, Chuki Shabani, alisema hali hiyo pia inasababisha wafanyabiashara wengi hususani wakubwa kuhamisha biashara zao katika mataifa mengine.
Alisema kwa sasa wanatakiwa kulipa Sh. milioni 2.7 kwa gari moja ikiwa ni gharama ya kodi kwa mwaka huku akiweka bayana kwamba kiwango hicho kinawakandamiza kibiashara.
Kutokana na hali hiyo, alishauri kushushwa hadi Sh. milioni moja na kwamba wamependekeza njia mbadala za ukusanyaji wa mapato ambazo zitaongeza kiwango cha ukusanyaji kodi bila kuathiri wafanyabiashara.
“Tunaiomba Wizara ya Fedha (na Mipango) kipitia Waziri Mwigulu Nchemba kama ameipata barua yetu, aijibu ili na sisi tuwajibu wasafirishaji wajue nini kinachoendelea kwa sababu mpaka sasa hawaelewi kitu gani kinaendelea.
“Watu wengi wenye uwezo wamehamisha biashara zao nchini kitu ambacho ni kibaya kwa uchumi wa nchi yetu. Sasa tunaomba kabla wengine hawajaikimbia nchi, ni vizuri tukakaa tukafikia mwafaka nini kifanyike ili kuondokana na tatizo hili,” alisema.
Aidha, alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan awasikilize kwa kuwa nia yao ni kujenga na kufikia malengo ambayo serikali imejiwekea bila kumuumiza mtu.
Pia alibainisha kuwa Tanzania kuna kodi nyingi ambazo hazikusanywi kupitia magari, hivyo akishauri kuwa serikali inaweza kukusanya kodi kupitia uchafuzi wa mazingira kutokana na moshi unaotokana na mafuta ya petroli za magari.
Alishauri kuwa endapo kikiwekwa kiwango cha Sh. milioni moja, kusingekuwapo na wafanyabiashara kukimbilia nchi za jirani, kwamba wangefanya usajili wa magari yao hapa nchini.
Kadhalika, alibainisha kuwa wanaunga mkono mchakato wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) wa kuwasajili madereva wa malori, licha ya kudai kuwa utaratibu na vigezo vilivyowekwa siyo rafiki kwa wahusika na kwamba inasababisha wengi kushindwa kusajiliwa.
Alishauri LATRA itumie namba za leseni za udereva kuwasajili madereva husika badala ya kuhitaji cheti ambacho kutokana na mazingira yao siyo rahisi kila mmoja kuwa nacho kwa sasa.
Pia aliishukuru serikali kwa kuwaunga mkono katika safari ya kwenda kutatua tatizo la foleni katika mipaka ya Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akieleza kuwa walipata ushirikiano kutoka kwa nchi hizo na kufanikiwa kumaliza tatizo.










