Mgomo huo ulitikisa mapato ya serikali kutokana na eneo la Kariakoo kuwa kitovu cha biashara, baadhi ya watu wanadai kuwa ndio uliomwondoa na kuhamishiwa Mwanza.
Safari hii, wamiliki wa hoteli, baa na kumbi za starehe jijini Mwanza wametishia kufanya mgomo leo kwa kufunga biashara zao. Wafanyabiashara hao wakishinikiza kuondolewa kwa faini na masharti magumu yaliyowekwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Masharti wanayolalamikia ni kuacha kupiga muziki uliopita vipimo, kulipia faini ya Sh.milioni tano pamoja na kununua kipima sauti kinachoelezwa kutokuwa na usahihi katika upimaji wake.
Endapo wafanyabiashara hao wakitimiza adhma hiyo, utakuwa ni mtihani wa pili anakutana nao Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla katika kipindi cha wiki mbili, wa kwanza alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam dhidi ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo.
Walitoa tamko hilo jana walipofanya kikao cha pamoja kujadili hatma ya shughuli zao baada ya kufungiwa kufanya wakitakiwa kulipia faini.
Joseph Gaspati, mmiliki wa hoteli ya Bundasliga alisema maofisa wa NEMC walichukua uamuzi wa kuwafungia huduma za muziki sambamba na kumweka mahabusu bila kupewa elimu yoyote juu ya vidhibiti sauti hivyo.
Alisema pia alitaliwa kulipa faini ya Sh. milioni tano kwa mkupuo ndani ya muda mfupi.
“Huo ni unyanyasaji. Kama hawataki tufanye biashara waseme tufunge hoteli zetu na faini hizo hatulipi. Pia ikifika Jumatatu (kesho) hatujafunguliwa shughuli zetu, tunafunga na watajua watakakopata mapato,” alisema
Ester John, mmiliki wa The Femurs Lounge, alisema utaratibu walioutumia NEMC haukuwa wa kistaarabu kutokana na kuwa wakati wa kuanzisha biashara hizo hakuna sehemu walipoelekezwa kuwa wanatakiwa kufika kwenye baraza kupewa sheria na taratibu juu ya upigaji muziki.
“Wengine uwezo wa kulipa faini kwa mkupuo hatuwezi kabisa na hili suala limekuja ghafla maana kama ni sheria na taratibu tulifuta zote lakini hatujawahi kuambiwa kuna utaratibu huu na licha ya hivyo tungeitwa kwanza tupewe elimu ndipo tuanze kutekeleza matakwa yao,” alisema.
Aidha, walisema ushirikiano kwa baadhi ya viongozi wa NEMC hauridhishi kutokana na kupewa majibu ya mkato, huku kauli yao ikiwa kutakiwa kulipia faini na kununua kifaa cha kupima sauti.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Patrick Msagati, aliwaomba wafanyabiashara hao wavumilivu kwa kipindi cha siku mbili wakati yeye na viongozi wenzake wakiendelea kufuatilia suala hilo.










