Diwani wa Kata hiyo, Abel Mbasa, amesema adha hiyo imekuwa ya muda mrefu na kuwalazimu watumishi hao kutumia gharama kubwa kufika shuleni.
Diwani huyo ametoa kilio cha Walimu hao kwa Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhandisi Deusdedith Katwale, kuwa baadhi ya walimu wanalazimika kwenda kuishi wilaya jirani baada ya shule zao kutokuwa na nyumba za kuishi huku jamii pia ikiwa haina nyumba zenye hadhi ya kuishi watumishi wa umma.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, kuhakikisha unakuwepo mpango mkakati wa muda mfupi na mrefu katika kutatua kero ya nyumba za walimu na madarasa.
Amesema mpango huo unatakiwa kuvipa kipaumbele Vijiji na Kata zilizoko mpakani mwa Wilaya hiyo, hali itakayosaidia kuinua kiwango cha elimu katika maeneo hayo.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mandia Kihiyo, amekiri kuwepo kwa adha hizo na kuahidi kuzitatua kwa kushirikiana na jamii husika ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha umuhimu wa kujenga nyumba bora za kupangisha ili kuinua uchumi wa Kaya.










