Wakaidi tahadhari Ebola kufungiwa biashara zao

09Oct 2022
Mary Geofrey
Bukoba
Nipashe Jumapili
Wakaidi tahadhari Ebola kufungiwa biashara zao

SERIKALI imesema itafunga biashara za wafanyabiashara ambao watakaidi kuweka vifaa vya kujikinga na tishio la ugonjwa wa Ebola katika mpaka wa Mutukula wilayani Misenyi mkoani Kagera.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Misenyi, Dk. Daniel Chochote, alitoa angalizo hilo juzi wilayani mwake wakati wa ziara ya kukagua utayari wa wafanyabiashara katika kujikinga na tishio la Ebola.

Dk. Chochote alisema tayari wametoa elimu ya kutosha na tahadhari wanazotakiwa kuzichukua ili kuepuka kupata maambukizi ya ugojwa huo.

"Kuanzia leo (juzi), wafanyabaishara wote watakaokaidi kuweka vifaa vya kunawia mikono nje ya maduka yao, wanasema hiari inashinda utumwa, tukifikia hapo tutalazimika kuwafungia maana bora kubaki na wafanyabiashara wachache ambao watahakikisha Ebola haiingii nchini," Dk. Chocholo alionya.

Alisema wamewataka wananchi wanaoingia na kutoka kuzingatia kanuni za afya ili ugonjwa huo usiingie nchini.

Diwani wa Mtukula, Swalehe Chakula alisema wameshatoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara na kazi inayoendelea ni kuhimiza waweke vifaa vya kunawa mikono nje ya biashara zao.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga, Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Dk. Ama Kasangala, alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini.

Dk. Kasangala aliahidi kuendelea kutoa elimu, kuweka mabango na vipeperusi pamoja na watumishi wa afya waliopo mipakani kuwapima wanaongia na kutoka nchini ili kuzuia ugonjwa huo.