Wadau hao ni Mtandao wa Kupinga Ukeketaji Tanzania, unaoundwa na mashirika zaidi ya 20wamezungumza na waandishi wa habari, katika ofisi za makao makuu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), jijini Dar es Salaam leo. Mkurugenzi wa shirika la C-SEMA, Michael Marwa, amesema ni muhimu kutungwa na kupitiaha sheria ya kuzuia ukeketaji ili kulinda wanawake watu wazima wanaokeketwa.
Aidha, amesema, Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni kikwazo, nayo irekebishwe kwa kuwa inachangia watoto kukeketwa na kuingizwa katika ndoa za utotoni.
"Lakini pia viongozi wa ngazi za juu serikalini wajitokeze wazi kuunga mkono jitihada za kutokomeza ukeketaji," amesema Marwa.
Aidha, amesema mtandao huo unashauri serikali kupitia wizara za kisekta kutenga bajeti ya utekelezaji wa mpango kazi wa kitaifa wa kutokomeza ukeketaji mwaka 2021 hadi 2024.
Pamoja na hayo, wameigusa jamii kuwa ikemee kwa nguvu zote vitendo vya ukeketaji na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, ikiwamo kutoa taarifa na ushahidi ili kufanikisha vita dhidi ya ukeketaji.
Ofisa Programu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Neema Kasabuliro amesema, ingawa kuna juhudi zinazofanywa na serikali, mashirika na taasisi mbalimbali, ukeketaji unaendelea kutekelezwa katika baadhi ya jamii.
"Takwimu za taarfa ya Demografia na Afya ya mwaka 2022, inaonyesha ukeketaji unaendelea kupungua, lakini kwa kasi ndogo.
Ofisa Mwandamizi, Jinsia, Wanawake, Watoto na Watu Wenye Ulemavu kutoka LHRC, Getrude Dyabene amesema zipo juhudi kubwa zimefanyika katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwamo mradi wa kutoa elimu na kusaidia watoto wa kike kukabiliana na mila ya ukeketaji.
"Lakini mtandao Bado unafanya kazi ya kuwezesha waathirika wa ukeketaji kufikia vyombo vya kisheria ikiwamo polisi na mahakama ili kuwachukulia hatua wale wote wanaoendeleza mila kandamizi," amesema Getrude.










