Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Eustard Ngatale, wakati akijibu hoja za wabunge kwenye semina ya wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), jijini Dar es Salaam jana.
Alisema suala la ujenzi holela halipo Tanzania peke yake,bali ni tatizo kwa dunia nzima, hivyo wabunge wanatakiwa kulisimamia ili halmashauri zifuate sheria.
Alisema ni lazima halmashauri ziwe zinachukua hatua ili kudhibiti ujenzi holela katika miji.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Kangi Lugola, alihoji sababu za halmashauri nyingi kutokuwa na mipango miji wakati zina maofisa mipango miji.
Aidha, Lugola alitaka fedha za Mfuko wa Jimbo zitengewe akaunti yake badala ya kuchanganywa na akaunti nyingine za halmashauri. Wajumbe hao wa Kamati ya LAAC na PAC walipewa semina kuhusu majukumu ya Tamisemi na usimamizi wa shughuli zake na muundo na majukumu ya Ofisi ya Rais Tamisemi.
Wabunge hao pia walijifunza sheria mbalimbali za serikali za mitaa, ikiwamo sheria ya mamlaka za serikali za mitaa sura 288 na Sheria za Leseni za Vileo Sura 77.










