UVCCM wahamasishana kugombea

29Feb 2024
Steven William
MUHEZA
Nipashe
UVCCM wahamasishana kugombea

​​​​​​​UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umewataka wanachama wake kujitokeza kwa wingi kugombea uongozi ndani ya umoja huo katika maeneo yao.

Wito huo ulitolewa na Makamu Mwenyekiti wake, Rehema Omari, wakati akizungumza na wanachama wa UVCCM na wa CCM wilayani hapa Mkoa wa Tanga.

Ni baada ya kufungua tawi la vijana wa UVCCM  Mlimani Park liliopo Mtaa wa Mdote Kata ya Majengo wilayani hapa.

 Rehema amesema wanachama wa umoja huo wanatakiwa kutambua kuwa wana nafasi nyingi kugombea ndani ya umoja huo kwa ajili ya kuimarisha CCM.

Amesema kila mwanachama wa jumuiya ana haki ya kugombea nafasi hizo na wakati ukifika wachukue fomu na kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpigakura.

"Na sisi tukiwa kama viongozi wenu tutahakikisha tunasimama imara kuhakikisha nafasi hizo vijana wanazipata," amesema Omari.

Ameongeza kuwa inatambulika kuwa hakuna kiongozi bora atakayepatikana kama hajapitia tanuri la UVCCM na kwamba jumuiya hiyo ndio inayoandaa vijana ambao ni taifa la kesho na wa siku zijazo.

Katika hatua nyingine; kiongozi huyo aliwaagiza Katibu Tawala Wilaya ya Muheza, Mohamed Mfaki na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dk. Jumaa Mhina kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri itakapotoka wapewe kipaumbele wanachama wa UVCCM wa shina hilo.