Akizungumza kwenye warsha ya wanahabari leo kuelekea kwenye utabiri wa kesho wa mvua za masika, Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladislaus Chan'ga, amesema utabiri wao wa mvua za vuli walioutoa mwezi Septemba mwaka jana umetoa matokeo chanya kwa kuwa sahihi kwa asili hizo.
Amesema mrejesho wa mvua hizo ambazo zilitabiriwa kuwa wastani mpaka juu ya wastani umeonyesha maeneo mengi yanayopata mvua hizo kupata mvua kwa kiwango kikubwa.
"Tulitabiri kuwa na mvua za juu kwenye maeneo mengi ya nchi, na kweli kulitokea hivyo na kupelekea athari mbalimbali kwenye maeneo hayo kama tulivyoshuhudia," amesema Dk Chang'a.
Aidha, amesisitiza uzingatiaji wa taarifa za hali ya hewa hususani tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa ni muhimu sana katika kuokoa maisha ya watu na mali zao na kuongeza tija katika ufanisi katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
"Kiwango cha usahihi wa utabiri kinazidi kupanda, ni vizuri kwa wananchji na mamlaka mbalimbali kufuatilia na kuchukua hatua kila utabiri unapotolewa hili kuepuka madhara yanayoweza kutokea," alisema Dk Chang'a na kuongeza.
"Kesho tunatarajia kutoa utabiri wa mvua za masika ambazo hizi ni mahususi kwa mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka, wananchi wafuatilie taarifa tutakazozitoa na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta mbalimbali," alisema Dk Chang'a.
Utabiri huo utakaotolewa kesho utaihusu mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Pwani, baadhi ya maeneo ya Morogoro na Mafia.
Pia itaihusu Kanda ya ziwa ikijumuisha mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Shinyanga na maeneo ya kaskazini ya mkoa wa Kigoma.
Pia Kanda ya Kaskazini ikijumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.










