Uhaba wa sukari kaa la moto

22Feb 2024
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Uhaba wa sukari kaa la moto

UHABA wa sukari umeendelea kuwa kaa la moto huku wakuu wa wilaya na mikoa wakiagizwa kusimamia kwa umakini katika maeneo yao usambazaji wa sukari iliyoingizwa kutoka nje ya nchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa.

Kutokana na nchi kukabiliwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo, hivyo kusababisha kuuzwa kwa magendo na bei ya juu katika baadhi ya maeneo, serikali ilichukua hatua ya kuagiza kutoka nje ili kupunguza makali kwa wananchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, aliwaagiza wakuu hao wa wilaya na mikoa kusimamia kwa umakini usambazaji wa sukari sambamba na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote wanaohujumu upatikanaji wake.

Mchengerwa alitoa agizo hilo katika ofisi ndogo za wizara, Magogoni jijini Dar es Salaam huku akisema serikali kupitia Tangazo la Serikali namba 40 lililotolewa  Januari, mwaka huu, lilitoa bei elekezi na kuwataka viongozi wote wa mikoa na wilaya kusimamia bei hiyo iliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwenye maeneo yao.

"Katika kukabiliana na upungufu wa sukari, serikali kupitia Wizara ya Kilimo iliruhusu uagizaji wa sukari ambapo zaidi ya tani 100,000 ziliingizwa nchini na utaratibu wa upatikanaji wa mawakala wa kusambaza sukari unaratibiwa kwenye ofisi za makatibu tawala katika kila mkoa.

"Hivyo majina ya mawakala walioruhusiwa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo kusambaza sukari katika kila mikoa, yameshatumwa kwenye ofisi za wakuu wa mikoa yote nchini chini ya usamamizi wa makatibu tawala, hivyo jukumu kubwa limebakia kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha mnasimamia usambazaji na uuzaji wa sukari kote nchini," alisema Mchengerwa.

"Hakikisheni mnashirikiana na Bodi ya Sukari chini ya Wizara ya Kilimo kuwakamata wafanyabiashara wote wanaokwenda kinyume cha maelekezo ya serikali na maelekezo ya Tangazo la Serikali.

“Pia taratibu za kijinai hasa zinazohusu masuala ya uhujumu uchumi zichukuliwe kwa mfanyabiashara yeyote anayekiuka misingi ya Taifa letu," ameeleza  Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa alisema hatarajii kuona mkuu wa mkoa au wilaya yeyote akishindwa kusikiliza kero za wananchi na kushindwa kutoa taarifa ya namna serikali inavyoendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.

Tangu kuanza mwaka 2024, kilio cha uhaba wa sukari kilisikika kila kona ya nchi huku baadhi ya wafanyabiashara kwenye maeneo mbalimbali wakikamatwa kwa madai ya kuficha na kulangua sukari.

Uhaba huo ulielezwa unatokana na baadhi ya viwanda vinavyozalisha sukari nchini kufanya matengenezo ya mitambo na miundombinu ambayo hufanyika kila mwaka, hivyo kusababisha kuwapo kwa tatizo hilo.

Kutokana na kuwapo kwa tatizo hilo, serikali ilichukua hatua kwa kutafuta kampuni kuagiza sukari nje ya nchi na hatimaye zaidi ya tani 100,000 zimeshaingizwa nchini ili kupunguza makali ya ukosefu wa bidhaa hiyo.

Siku za karibuni, kumekuwa na uhaba zaidi wa sukari, hivyo kusababisha athari mbalimbali ikiwamo kupanda bei kwa baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa kwa kutumia bidhaa hiyo.

Katika maduka machache ambayo bidhaa hiyo imekuwa ikipatikana, kilo moja ya sukari imekuwa ikiuzwa kati ya Sh. 4,000 na 5,000. Kabla ya kuadimika, bei katika mkoa wa Dar es Salaam ilikuwa kati ya Sh. 3,000 na 3,200.