TRA yafanikisha mkakati mzito

20Mar 2016
Christina Mwakangale
Dar
Nipashe Jumapili
TRA yafanikisha mkakati mzito

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), imewekeana saini makubaliano ya kutekeleza mpango wa kudhibiti upitishwaji wa makontena ya mizigo (CCP), ili kudhibiti wizi, upitishwaji wa bidhaa za magendo na utoroshwaji wa mizigo.

Waziri wa Fedha Dkt. Phillip Mpango kushoto.

Aidha, mpango huo utatekelezwa na idara pamoja na taasisi nyingine za serikali ikiwamo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Jeshi la Polisi, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) pamoja na Chama cha Wanyapori Tanzania.

Utiliwaji wa saini huo ulifanyika juzi jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa TRA, Mary Maganga na Mwakilishi mkazi wa Afrika Mashariki katika Kudhibiti Makontena, Wanyamapori, Misitu na Uhalifu (UNODC), Jamier Montano.

Akizungumza mara baada ya kuweka saini katika mpango huo, Maganga alisema kumekuwa na matukio ya uhalifu ambayo yanatokea kupitia bandari na mipaka ya nchi zikipitishwa silaha pamoja na magari yaliyotoroshwa.

“Kabla ya uwekaji wa saini, kulikuwa na mafunzo waliyopewa wawakilishi kutoka taasisi na idara hizi, ili kuwapa ujuzi namna ya kukabiliana na masuala ya uhalifu, wakiwa katika mafunzo wiki mbili tu waliweza kubaini wizi wa gari lililokuwa linapelekwa Kigali nchini Rwanda, baada ya kuibiwa bandarini,” alisema Maganga.

Naye mwakilishi wa UNODC, Montana alisema uwekaji saini huo unaonyesha namna ambavyo jumuiya za kimataifa zinaweka mkazo na jitihada za kupambana na uhalifu pamoja na upitishwaji wa magendo katika bandari na mipaka ya nchi.

“Bidhaa za magendo kama pembe za ndovu, dawa za kulevya, na vingine na kuhatarisha usalama wa nchi ni matarajio yetu mpango huu utasaidia,” alisema Montana.

Naibu Kamishna wa Operesheni Maalum wa Jeshi la Polisi, Daniel Nyambabe alisema kuwa kunahitajika vyombo vya kisasa na teknolojia ya kisasa ili kupambana na uhalifu wa mipakani pamoja na bandarini.

Alisema hatua hiyo inaonyesha namna serikali ilivyo tayari katika kudhibiti uhalifu ikiwamo bidhaa za magendo, dawa za kulevya na wizi wa bidhaa kama magari.