TIC kupata Tril. 4.3/- miradi ya kimkakati

25Jun 2023
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
TIC kupata Tril. 4.3/- miradi ya kimkakati

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesaini mikataba ya utekelezaji wa miradi iliyopewa hadhi ya kimkakati yenye thamani ya Dola bilioni 1.8 (Sh. trilioni 4.3)  ambayo inatarajia kutoa ajira zipatazo 16,355.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri, alisema utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji ni kati ya TIC na miradi iliyopewa hadhi ya kimkakati na Kimkakati Mahiri na Kamati ya Taifa ya Uwekezaji (NISC).

Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni wa kongani ya viwanda wa Sinotan unaotekelezwa Kwala, mkoani Pwani.

“Mradi huu unatarajia kuwa na uwezo wa kuwa na viwanda zaidi ya 200 ndani ya mradi utakapokamilika. Utakapokamilika unatarajiwa kugharimu Dola milioni 327 na kuleta ajira zipatazo 2000 za moja kwa moja na 50,000 ambazo si za moja kwa moja,” alisema.

Mingine aliitaja kuwa ni mradi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero unaotekelezwa mkoani Morogoro, ukihusisha upanuzi na wa kilimo cha miwa unaogharimu Dola milioni 238.5 na kuleta ajira mpya zipatazo 1404 za moja kwa moja na 15,000 ambazo siyo za moja kwa moja.

“Mradi wa WILMAR unaotekelezwa Kihonda Morogoro, ni wa viwanda na uchakati wa nafaka na utakapokamilika unatarajiwa kugharimu Dola milioni 51.5 na kuleta ajira mpya zipatazo 360 za moja kwa moja na 1,000 ambazo si za moja kwa moja.  Kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 271,000 za mchele na hivyo kupunguza mahitaji ya uagizwaji kutoka nje,” alisema.

“Mwingine ni Mradi wa Upanuzi wa kiwanda cha uzalishaji wa saruji wa Lake Cement unaotekelezwa Kigamboni Dar es Salaam, ambao hadi sasa umewekeza Dola milioni 101,” alisema

Teri alitaja mwingine ni wa kusindika na kuhifadhi gesi ya LPG na miundombinu ya gesi wa Oilcom unaotekelezwa Dar es Salaam unaogharimu Dola milioni 111.87 na kuleta ajira zipatazo 1600 za moja kwa moja 160,000 zitakazotokana na mnyororo wa thamani.

Aliitaja mingine ni Mradi wa Wild Flower and Oil Mills unaotekelezwa Manguanyuki Singida wa Dola milioni 24.

“Mradi wa Mufindi Paper Mills unatekelezwa mkoani Kigoma kwa ajili ya kilimo cha miwa na kiwanda ili  kuzalisha sukari  unagharimu dola milioni 320.

“Mradi wa Lodhia Steel unaotekelezwa Mkuranga mkoani Pwani utakaozalisha mabati ni wa Dola milioni 45, mradi wa Dangote Cement unaotekelezwa mkoani Mtwara na mradi wa Mount Meru Millers unaotekelezwa mkoani Singida,” alisema.