Wanawake wa TFRA jana, waligusa mioyo ya wasichana 110 kutoka mikoa mbalimbali wanaosoma Sekondari ya Jangwani kwa kuwapa mahitaji ya usafi na ya kitaaluma, yenye thamani ya zaidi ya Shilingi 2,000,000 pamoja na kuwaandalia chakula cha mchana.
Akizungumza katika hafla ya kusherehekea na wasichana hao, iliyofanyika shuleni hapo, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi TFRA, Victoria Elangwa, aliwapongeza wanafunzi hao kuthibitisha kuwa kuishi na ulemavu si kushindwa maisha.
Aliwasifu kwa juhudi zao kitaaluma kwa kusoma tahasusi za sayansi, uchumi, hesabu,biashara na sanaa na kuwaeleza kuwa wajitahidi kwani ndiyo sehemu ya wataalamu wa taifa hilo kesho.
Aliwaambia kuwa katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani, TFRA inaunga mkono juhudi za serikali katika kuchangia maendeleo ya Watanzania maeneo mbalimbali zikiwamo taasisi za elimu.
Aliwataka kuongeza juhudi darasani ili kuwa wataalamu na raia watakaoitumikia na kuiendeleza nchi kwa ufanisi.
Baadhi ya vifaa walivyopokea wasichanao hao kwa mujibu wa Victoria ni daftari, kalamu, mikebe ya vifaa vya hesabu, karatasi (rim papers), sabuni, karatasi za chooni, mafuta ya kupaka, mafagio na madekio.
Aliwaambia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea inawaunga mkono na kuwasaidia mahitaji ili kuwaendeleza kitaaluma na kushirikiana wazazi, wanafunzi wenye mahitaji maalumu na walimu kutimiza azma ya serikali ya kutoa elimu bora.
Kwa upande wake, Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano, Matilda Kassanga, alisema taasisi hiyo ya umma inawajibika kujenga na kushiriki juhudi hizo ili kuimarisha uhusiano kati ya TFRA na wadau wakiwa taasisi za serikali na binafsi zikiwamo zinazotoa elimu.
“Tunalenga pia kurudisha shukrani zetu na kuwajibika kwa jamii, kutoa hamasa kwa watoto hawa katika masomo yao ili wafanye vizuri zaidi na kuwa mfano,” aliongeza Matilda .
Alisema wanatambua kuwa wasichana hao ni wamama wa kesho, lakini pia ni wataalamu wa fani mbalimbali wanaotegemewa na taifa, hivyo wanawake TFRA ni kuwapa hamasa zaidi kufikia mafanikio katika masomo yao .
“Tunapenda tuwe mifano kwao (role model) kuwahamasisha kufikia mafanikio kitaaluma na pia kuwa raia na wataalamu bora.” Alisema Matilda.
Makamu Mkuu wa Sekondari ya Jangwani, Paulina Aweda, akiwashukuru wanawake wa TFRA, alisema sekondari hiyo inatoa elimu jumuishi inayohusisha wenye mahitaji maalumu.
“Wapo wanafunzi 1,360 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Tunashukuru TFRA kuwagusa na kushiriki juhudi za serikali za kuwapatia watoto wetu elimu bora.”
Alisema misaada hiyo ni chachu kwa wanafunzi na pia ni kuisaidia serikali kufikisha huduma za jamii kwa makundi yote wakiwamo wenye wahitaji maalumu.
Wasichana hao walionyesha vipaji vyao wakiimba na kutumbuiza wimbo ‘I know I can Be what I wanna be If I work hard at it I'll be where I wanna be…” ulioimbwa na msanii wa Amerika Nasir Bin Ulu Dara.