Sh. bilioni 11 za kifisadi zarejeshwa serikalini

29Jan 2016
Salome Kitomari
Nipashe
Sh. bilioni 11 za kifisadi zarejeshwa serikalini

OFISI ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), imewezesha serikali kupata zaidi ya Sh. bilioni 11, yakiwamo magari ya kifahari saba, nyumba na kiwanja kutokana na kesi za uhujumu uchumi.

Mali hizo ni zilizopatikana kupitia kesi zinazohusiana na uhalifu na udanganyifu wa kujipatia mali kwa njia haramu, kama kusafirisha wanyamapori, rushwa, dawa za kulevya na usafirishaji haramu binadamu zilizoamuliwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mbeya na Kilimnajaro.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, DPP Biswalo Mganga (pichani), akiwa amembatana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Alex Mfungo, alisema kesi hizo zimefanikiwa kwa ushirikiano na taasisi za kimataifa ikiwamo Benki ya Dunia (WB).

Alitaja baadhi ya kesi kuwa ni kiwanja kilichoporwa kwa rushwa kilichopo karibu na Hospitali ya Akha Khan, jijini Dar es Salaam, raia wa kigeni aliyekutwa na mfupa wa Twiga ambaye alilipa faini ya Sh. milioni 64.38 na mwingine alikutwa na pembe mbili za twiga ambaye alitozwa Sh. milioni 64.

DPP Mganga alisema kesi nyingine ilihusu raia wa Afrika Kusini aliyekutwa na meno manne ya kiboko na mamba na kulipa faini ya Sh. milioni 68.16, raia wa China wawili waliokutwa na meno 11 ya tembo ambao walifugwa miaka 20 na kutakiwa kulipa Sh. bilioni 9.288 na gari lao kuitaifishwa.

Nyingine ni iliyomuhusu mkazi wa Mpanda aliyehukumiwa miaka 30 na kulipa faini ya Sh. bilioni 1.2, aliyekutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya raia wa Kenya ambaye alihukumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na kutozwa faini ya Sh. milioni 162 na Mtanzania aliyetozwa faini ya Sh. milioni 143 na kifungo cha maisha.

“Tunataka Watanzania na wageni wajue kuwa Tanzania siyo mahala pa kufanya uhalifu na kujipatia utajiri. Sote tumsaidie Rais ili nchi iwe kisiwa salama,” alisema.