Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema ofisi yake tayari imepata kibali kutoka Utumishi cha kuajiri watumishi 23,000 kwa kada hizo.
Mchengerwa, amesema hayo wakati akifunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu na Maofisa Elimu wa Halmashauri nchini, kikao kilichofanyika kwa muda wa siku tatu mjini Morogoro.
Amesema Tamisemi imepata kibali cha ajira mpya kwa kada ya elimu na afya, huku lengo likiwa ni kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu na wahudumu wa afya nchini.
Mchengerwa, amesema kuwa baada ya kupata kibali hicho, ajira hizo zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni na kufunguliwa kwa dirisha ya maombi.
"Tayari Tamisemi tunachokibali cha ajira na tutatangaza hivi punde ajira za walimu na maofisa afya karibu 23, 000 wataajiriwa" amesema Waziri Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa, amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa serikali ya awamu ya sita ya kuajiri walimu ambapo mwaka 2022/2023, jumla ya walimu 13, 130 waliajiriwa na kupangiwa katika maeneo mbalimbali yenye upungufu wa walimu nchini.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Makatibu Tawala Wasaidizi Elimu na Maofisa Elimu wa Halmashauri nchini, Ofisa Elimu wa mkoa wa Tabora, Juma Kaponda, aliipongeza serikali ya awamu ya sita kupitia Utumishi kwa kutoa kibali cha ajira kwa Tamisemi cha kuajiri walimu ili kupunguza uhaba uliopo kwenye shule za msingi na sekondari.
“Tumefurahishwa na jitihada zako za Waziri wetu kwa kutusaidia hizi ajira za walimu,tunaomba Mungu ingekamilika Januari hii badala ya mwezi Februari mheshimiwa Waziri “ amesema Kaponda
Kwa niaba ya washiriki wenzake, Kaponda amesema kwa sasa sekta ya elimu ipo kwenye mikono salama chini ya Waziri Mchengerwa kutokana na jitihada zake za kuwatetea walimu na wanachokiahidi kwake ni kutimiza majumu yao ipasavyo kwenye usimamizi wa sekta ya elimu nchini.










