... zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Akizungumza na gazeti hili katika ofisi za Halmashauri ya wilaya, Mkuu wa Wilaya hiyo Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Mbaraka Batenga, alisema kuwa ukame mwaka jana uliiathiri kwa kiasi kikubwa Wilaya hiyo na kuwapa hasara kubwa wafugaji na wakulima.
Alisema kufuatia hali hiyo Kamati ya maafa ya wilaya hiyo iliamua kuanzisha utaratibu wa kusambaza taarifa za hali ya hewa za TMA kwa wakulima na wafugaji kwa njia ya simu na mikutano.
“Kwa sasa wilaya yetu kuanzia ngazi ya serikali ya wilaya mpaka kwa wakulima na wafugaji tunazifuatilia kwa karibu taarifa zote za TMA kuanzia ule utabiri wao wa siku wiki mpaka mwezi pamoja na utabiri wa msimu, lengo ni ujaribu kujitahadharisha kwa hali yoyote mbaya ambayo tunaweza kukutana nazo kwenye kila msimu,” alisema Batenga.
Akifafanua zaidi, alisema wameanzisha makundi ya mtandao wa simu ya ‘Whatsapp’ kwa baadhi ya wakulima, wafugaji watendaji na wenyeviti wa vijiji wenye simu za smati ambao nao wanasaidia kuwapatia wengine wasio na simu hizo taarifa muhimu za hali ya hewa.
"Hii yote inatokana na ukame ambao tulikutana nao msimu uliopita, mazao kunyauka na sehemu nyingine kutoota kabisa, lakini pia baadhi ya maeneo yetu yanapakana au yapo ndani ya eneo la hifadhi ya asili ya Makame, tumeshuhudia wanayama pori wakifariki kwa kukosa malisho na maji,” alisema Batenga.
Alisema kwa wafugaji walipata hasara kubwa ambapo jumla ya mifugo 25,000 ilikufa kwa kukosa maji na malisho kufuatia ukame huo.
Aidha, Afisa wanyamapori wa Wilaya Dorice Gama, alisema vifo vya wanyama pori na mifugo ilitokana na hali ya kugombania maji yaliyokuwa kwenye mabwawa na visima vichache vya sili kati ya mifugo, wanyama pori na binadamu.
“Hii kwetu imekuwa kama funzo, kwa sasa kuna visima na mabwawa ambavyo vimechimbwa na vimejaa maji msimu huu kutokana na mvua iliyonyesha, hii itasaidia kuwa na uhakika wa maji kwa muda mrefu,” alisema Dorice.
Aidha, Mkuu wa wilaya Batenga, alisema kwa sasa wilaya hiyo ina mifugo 1,350,000 ambapo ng’ombe wapo 500,000, Mbuzi 480,000 na kondoo 370,000.










