Samia Suluhu: Serikali na Sekta binafsi zitatue umaskini wa watu

16Apr 2016
Romana Mallya
Dar
Nipashe
Samia Suluhu: Serikali na Sekta binafsi zitatue umaskini wa watu

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu, amesema Serikali na sekta binafsi kwa pamoja zina mchango wa kushughulikia changamoto nzito na ngumu zinazolikabili taifa kwa kupanua fursa muhimu kwa watu maskini ikiwa ni pamoja na kuyafikia Malengo Endelevu ya Milenia (SDGs).

makamu wa Rais, Samia Suluhu.

Samia alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mkutano wa mwaka wa kwanza wa kuangalia mchango wa sekta binafsi/biashara binafsi katika kuleta maendeleo endelevu Tanzania.

Alisema wakati serikali ikitekeleza malengo ya SDGs waliyoyaweka Umoja wa Kimataifa (UN) inategemea mchango mkubwa wa utekelezaji wake kupitia sekta binafsi.

“Wakati tunatekeleza malengo ya Milenia (MDGs) serikali iliyatekeleza kwa nguvu zake yenyewe na kuacha sekta binafsi, sasa tunapotekeleza SDGs msukumu ni kwamba serikali, sekta binafsi, taasisi za kijamii zinatakiwa kushiriki kikamilifu ili tuweze kufikia pale tunapotakiwa,” alisema.

Alisema kupitia mkutano huo wanaamini utazaa mingine baada ya kampuni na sekta binafsi zitakapojadili jinsi sitakavyojiandaa kwa kuangalia mapungufu yao na uwezo wao ili washirikiane na serikali.

“Hata kama yupo mwenye kufikiria mabadiliko ya tabia nchi, kupunguza umaskini au kutoa nishati, chakula na maji kwa watanzania milioni 45, ni dhahiri kwamba sekta ya biashara lazima iwe msingi katika kutimiza wajibu huo,” alisema.

Alisema kama ilivyo nchi nyingine, serikali haiwezi peke yake kukidhi mahitaji ya kijamii ya watu wenye rasilimali bila ya mchango wa sekta binafsi katika kupanua huduma za jamii.
Alisema serikali imedhamiria kujenga mazingira mazuri ya biashara na sekta nyingine ili zijisikie huru kujadili kuhusu masuala endelevu ya maendeleo.

Alisema serikali imejitoa kuimarisha mipango maalum ya kwenye tasnia kama ule wa uwazi wa kuimarisha mapato yatokanayo na sekta ya madini.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa African Sustainable Business, Raymond Mubayiwa, alisema wanategemea mchango wa sekta binafsi katika kuyafikia malengo ya MDGs

Mratibu Mkazi wa UN na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNDP),Alvaro Rodriguez, alisema malengo ya SDGs ni muhimu kwa sababu yatategemea maendeleo ya miaka 15 ya nchi kwa baadaye.
Alisema ni wajibu wa sekta katika mafanikio ya SDGs kwa sababu serikali peke yake haiwezi kuyafikia.

“Mafanikio chanya baina ya serikali na sekta binafsi ni msingi muhimu wa kufikia mafanikio endelevu ya SDGs kwa sababu ya mahitaji ya kifedha na ya kimkakati,” alisema.

Kwa mujibu wa makadirio ya ripoti ya Kamati inayojumuisha wataalamu wa pande zote katika maendeleo endelevu ya kiuchumi, nchi zote zinatakiwa kuwekeza dola za kimarekani trilioni 5 hadi 7 kwa mwaka hadi kufikia 2030.