Aidha, ameonya matumizi mabaya ya mitandao kwa vijana na kuwataka watumie kwa kulinda mila, desturi na kujielimisha.
Akizungumza jana kwenye hafla ya kutia saini mikataba ya ujenzi wa minara 758 kati ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na watoa huduma ya mawasiliano nchini, Rais Samia alisema kuna urasimu kwenye utoaji vibali vya ujenzi minara na imekuwa ikichukua miezi sita mchakato wa kibali.
“Sasa tutaitana na wote wanaohusika na mambo haya ya kutoa vibali, vibali hivi vya minara iliyosainiwa leo visizidi zaidi ya mwezi mmoja vibali vyote viwe vimetoka, kuanzia leo hadi Juni 13 nitamuuliza Waziri wamekwama wapi nani amekwamisha.”
“Kwa hiyo wale wenye makoti mazito ambayo hayainui mikono kwenye kutoa vibali yainuliwe yawekwe kwenye viti ili mikono iwe myepesi kutoa vibali kisheria kulingana na kanuni tulizojiwekea,”alisema.
Kuhusu tozo zinazolalamikiwa na watoa huduma na kusababisha mabando kuwa ghali, Rais alisema tozo ya kupitisha mkongo kwenye eneo la akiba ya barabara inalalamikiwa ambayo ni Dola za Marekani 1,000.
“Kuna taasisi kadhaa zinatumia maeneo yale tozo zipo chini lakini mkongo ni Dola za Marekani 1,000 kupitisha kwenye maeneo hayo. Sasa hii haiwi bure inakwenda kuingia kwenye gharama za mabando za watu wa simu, ili tushushe gharama na watu wetu wakatumie vizuri huduma kule vijijini lazima serikali tuliangalie hili vizuri,”alisema.
Kuhusu upungufu wa umeme maeneo ya vijijini ambako minara hiyo itajengwa, alisema: “Mnara mmoja kwa mwezi unatumia Sh.Milioni 1.8 tukitumia majenereta lakini tukitumia umeme tunakwenda kutumia Sh.400,000 tu, kwa hiyo tunapaswa kulitazama suala la umeme vijijini.”
Aliagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha minara hiyo inakuwa na umeme ili kushusha gharama za bando na lisiposhuka watakamatana na watoa huduma.
FAIDA ZA MINARA
Rais Samia alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ambayo amekuwa akitoa mara kadhaa ya kukuza na kuimarisha sekta ya Tehama kwa vijana na kusukuma maendeleo.
“Kuwapo kwa huduma bora za mawasiliano hususan vijijini ni muhimu sana kiuchumi, kisiasa, kijamii, ulinzi na usalama wa nchi, ujenzi wa minara hii ni kichocheo kikubwa cha mafanikio kutokana na wananchi wote kuguswa na kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi,” alisema.
Alisema uwekezaji huo utakuza biashara vijijini na kadhia ya ukosefu wa mtandao inakwenda kuondoka kwa wakulima na wananchi wa maeneo hayo.
“Tunakwenda kubadilisha teknolojia vijijini kwa sasa wakulima wana visimu vya tochi, tukiimarisha mitandao yetu ya mawasiliano wakulima wanakwenda kutoka kwenye tochi wanakwenda kwenye ‘touch’ (simu janja) kwa sababu zile za touch zitawapa taarifa zote za nchi na za kidunia,”alisema.
Pia, alisema hatua hiyo inakwenda kuimarisha huduma za matibabu mtandao vijijini na kupunguza vifo vya wanawake na watoto wakati wa kujifungua.
Kuhusu huduma za TEHAMA shuleni, Rais Samia aliagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenye kongamano la sera na mitaala mipya ya elimu kulipeleka suala la TEHAMA ili kupata maoni kwa wananchi.
Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alizitaka kampuni za mawasiliano hapa nchini kuendelea kuwekeza na kuongeza mitaji ya uwekezaji wao ili kuimarisha mawasiliano nchini.
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alisema kumekuwapo na malalamiko kuwa mawasiliano ni ghali hasa kwenye simu janja na bando.
Aliomba Serikali kuangalia namna ya kupunguza tozo za kupitisha mkongo wa taifa ambazo ni dola za Marekani 1,000 na kusema gharama hizo zimekuwa zikichangia kuongezeka ghamara kwa wananchi.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari, Nape Nnauye, alisema kupitia UCSAF imefikisha mawasiliano kwa watanzania zaidi ya milioni 15 wanaoishi vijijini.
“Hadi sasa UCSAF imeingia makubaliano na kampuni za kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kata 1,258 zenye jumla ya vijiji 3,704 na wakazi milioni 15.1, jumla ya minara ya mawasiliano 1,380 itajengwa katika mikataba 19 ambayo mfuko umeingia na watoa huduma za mawasiliano,”alisema.
Alisema serikali imetoa ruzuku ya Sh. Bilioni 199.9 na ni ushahidi wa jinsi serikali inavyothamani na kuhakikisha kuwa watanzania hasa wa vijijini wanapata huduma za mawasiliano.
Nnauye alisema asilimia 93.4 ya miradi iliyotangazwa imechukuliwa na kwamba awali ilikuwa inaishia asilimia 60.
“Tulitangaza zabuni za minara 763 tumepata watoa huduma katika kata 713 sawa na asilimia 93.4, katika kata 50 zilizobaki tutakaa chini na watoa huduma nina hakika watoa huduma watafikiria kuzichukua hizi kata changamoto ni kwamba zina wakazi kidogo nao wanahitaji huduma hii,”alisema.
Waziri huyo alisema serikali kupitia UCSAF imekuwa ikitoa ruzuku ya asilimia 40 na watoa huduma huchangia asilimia 60 iliyobaki ya mradi.
“Gharama za kujenga mnara mmoja ni Sh. Milioni 300 hadi 350. Hata hivyo gharama zote za uendeshaji wa minara hii huwa inabaki kwa watoa huduma ambayo ni wastani wa milioni 2.5 kwa kila mnara unaojengwa,”alisema.
Alisema serikali imedhamiria kuhakikisha huduma ya mawasiliano inapatikana kote nchini ifikapo mwaka 2025.









