Vilevile, mradi huo unatarajiwa kutoa ajira 10,000 kwa kipindi cha ujenzi na baadaye za kudumu 500 na ndiyo sababu ya uamuzi wa serikali wa kuanzishwa kanda maalum ya kiuchumi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vyenye muunganiko na mradi.
Mkuu wa Nchi alibainisha hayo jana Ikulu Chamwino baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya awali ya mkataba wa mradi wa nchi hodhi wa kuchakata na kusindika gesi ya LNG baina ya Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni za Shell na Equinor zilizogundua nishati hiyo kwenye kitalu namba moja, mbili, nne na kina cha Bahari ya Hindi.
Alisema mradi huo wa kimkakati ni mahususi kwa kuwa unaleta mtaji na mapato nchini na kwamba utakapokamilika utabadilisha taswira ya uchumi wa nchi, huku akitoa maelekezo sita.
Rais katika agizo lake kwa kwanza, aliwataka watendaji wanaohusika kwenye majadiliano, kusimamia maslahi ya nchi kwa kuhakikisha kunakuwa na wepesi kwa kila upande.
La pili, mikoa ya Lindi na Mtwara kujiandaa kuzitumia fursa zitakazoletwa na mradi katika kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Tatu, Rais aliagiza mchakato wa majadilino na makubaliano ujenge uwezo wa Watanzania ili vizazi vijavyo vivune kwa tija na kujitegemea zaidi.
Nne, lazima kujenga uwezo wa Watanzania kushiriki kikamilifu na kutumia manufaa ya mradi na kwamba mafuta na gesi ni biashara na uwekezaji mkubwa unaohitaji kuimarisha taasisi za umma ili kusiwe na kikwazo kwa kuwa walindaji wa mradi ni Watanzania na siyo wawekezaji.
La tano, TPDC ndiyo wabia, hivyo wanapaswa kuwa shirika la kimkakati kwa nchi ili miaka ijayo shughuli hizo wazifanye wenyewe, Rais Samia akifafanua kuwa uzoefu wa sasa unaonyesha hakukuwa na wataalamu wa kutosha hadi wakatafutwa kwingine.
“Huko mbele tuwe nao na ndiyo maana nimeweka Mwenyekiti wa bodi nzito, Balozi Ombeni Sefue, atakayeweza kusimamia vyema TPDC, pia waziri naye ameweka bodi nzuri.
“TPDC kazi iko kwenu, nyie ni wachezaji, tunategemea magoli mengi kutoka kwenu, iwapo hamasa. Wizara ya Nishati wakae na Wizara ya Fedha waone namna gani ushiriki wa TPDC uwe wenye manufaa, tumewapa kazi, lazima wapewe nyenzo za kuifanya kazi vizuri," aliagiza.
Katika agizo lake la sita, Rais Samia alisema Watanzania wajipange kunufaika na fursa kwa kuwa mbali na mtambo wa kuchakata gesi, kutakuwa na kanda maalum ya uchumi, hivyo sekta binafsi lazima ijipange kutoa huduma kwenye mradi, kuhudumia mradi wenyewe katika kukuza uchumi badala ya kusubiri watu wa nje waje kutoa huduma kwenye mradi na kupeleka mapato kwingine.
“Sekta binafsi ihusike kwa sababu uzoefu unaonyesha maeneo ambayo serikali inaendesha yenyewe, hakuna utekelezaji mzuri. Kutia saini mkataba haina maana uwekezaji utaanza kesho kwa kuwa bado kuna vipengele vinahitaji mjadala, ni matumani ikifika Desemba mwaka huu tutasaini makubaliano ya pili mradi uanze na kwenda kwenye hatua nyingine," alisema.
Kwa mujibu wa Rais Samia, mradi huo utagharimu Sh. trilioni 70 na asilimia 10, yaani Sh. trilioni saba zitatumika ndani kwa ununuzi na kutoa huduma ndani ya nchi na hivyo kuwa fursa pana kwa Watanzania kiuchumi.
Alisema kuna fursa nyingine ya mradi kwa gesi kutumika nyumba na kwenye huduma za kijamii na maboresho makubwa yatafanyika kwa Uwanja wa Ndege Mtwara, barabara na huduma za kijamii kwa kuwa na shule, vituo vya afya vizuri, maji na umeme.
Awali Waziri wa Nishati, Januari Makamba, alisema ugunduzi huo wa gesi ulifanyika kwa kushirikiana na washirika na TPDC, serikali ikifanya uamuzi wa kuanza mradi wa kusindika na kuchakata gesi asilia kutoka kwenye hali ya hewa kwenda kwenye kimimnika kwa ajili ya kuuza nje na kutumia nyumbani.
“Utekekezaji mwa mradi huu Lindi utafanyika sambamba na uendelezaji wa miundombinu ili kuwezesha kuvuna rasilimali hiyo kwa ajili ya uendelezaji, tutajenga mtambo nchi kavu tofauti na nchi nyingine wanajenga kilipo kisima kwa kuweka meli ichakate na kusafirisha duniani.
“Tunajenga miundombinu kutoka nchi kavu itakapokuwa mtambo kwenda kilomita 100 hadi 160 halafu tunaenda kilomita tatu kufikia sakafu ya bahari na kuchimba kilomita mbili zaidi iliko gesi.
"Ni mradi mkubwa utakaobadilisha sura na taswira ya nchi, tumepata eneo Likongo, Mto Mkavu na Masasi ya leo mkoani Lindi tumeshalipa fidia kwa maridhiano kwa kaya 642 na tayari serikali ina hati.
“Uwekaji saini wa masuala muhimu yaliyokubalika katika hatua za awali na mengine yatawezesha usanifu wa kihandisi kufikia uamuzi wa mwisho ya uwekezaji mwaka 2025.
“Tanzania tuna visima 34 vya mafuta na gesi, vitalu 22 hakuna kinachoendelea, vitalu 12 ndiyo kuna shughuli, tunaamini mwaka ujao wa fedha na unaofuata kutokana na shughuli hii na hamasa, tutapata watu wengi zaidi kuja kuwekeza,” alisema.
Waziri huyo alisema dunia inahama kutoka kwenye gesi chafu kwenda safi na ya Tanzania ni asilia ambayo ni chafu kidogo, inayofaa kutumia kipindi cha mpito duniani, akiyataja masoko ya China, India, Korea na Japan ambayo kijiografia ni rahisi kuyafikia.
Wawakilishi wa kampuni za Equinor na Shell, walisema zaidi ya Sh. trilioni tisa zimewekezwa kwenye utafiti wa kiwango cha gesi asilia na ili kuifikisha nishati kwenye masoko makubwa duniani, ni lazima kufanya uwekezaji mkubwa kwa kujenga miundombinu nje na ndani ya bahari.










