Rugambwa: Nina mzigo mkubwa, niombeeni

08Oct 2023
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Rugambwa: Nina mzigo mkubwa, niombeeni

ASKOFU Mkuu Mwandamizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, amesema ana mzigo mkubwa wa kutimiza wajibu aliopewa huku akitaka waumini na Watanzania wamwombee.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Amesema kuteuliwa katika daraja hilo ni kutimia kwa kauli ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliyemtabiria siku moja kuwa, akirudi Tanzania atakuwa na nafasi kubwa bila kuitaja.

Akizungumza jijini Dar es Salaam muda mfupi baada kuwasili akitokea Vatican nchini Italia, Kardinali Rugambwa alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kurejea salama na kuomba aombewe ili kuyatenda yaliyo mema kulingana na vazi hilo alilovalishwa ambalo ni zuri.

Mapokezi ya Kardinali Rugambwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), yaliongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.  

Septemba 30, mwaka huu, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, aliwapandisha maaskofu wakuu 21 kuwa makardinali, akiwamo Rugambwa.

Kardinali Rugambwa alisema anashukuru Kardinali Pengo aliyemwambia mwaka 2012 kuwa wito aliopewa wa kuwa Balozi wa Papa akiufanya vizuri anaweza kurudi nyumbani akiwa na wadhifa mkubwa ambao wakati huo hakuutaja.

“Utabiri huu naona umetimia. Nimerudi  nyumbani nikiwa Kardinali. Ninakushukuru sana (Kardinali Pengo) kwa ushauri mbalimbali ulionisaidia katika majukumu yangu nikiwa Vatican.

“Kuvaa dera ni rahisi ila kazi kulishika. Leo hii nina wadhifa wa Kardinali mabegani mwangu. Jukumu langu kubwa kuyafanyia kazi hayo majukumu mapya niliyo nayo. Ni majukumu mazito, peke yangu siyawezi nahitaji sala zenu,”aliomba.

Kardinali Pengo alisema anashukuru kwa kupata msaidizi wa kazi hizo za kanisa na kuwaomba Watanzania kumwombea.

Alimkumbusha Kardinali Rugambwa kuwa nyakati fulani alimtabiria kuwa akifanya vizuri huenda akarudi nyumbani na madaraka makubwa.

 

 

Makamu wa Rais, Dk. Mpango, alisema Kardinali Rugambwa ameiletea sifa Tanzania na dhamira ya serikali ni kushirikiana na viongozi wa dini kuendeleza amani na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Alisema serikali itaendelea kushirikiana na kanisa hilo na madhehebu mengine kuleta maendeleo na kuhimiza umoja, amani na utulivu.

Dk. Mpango alisema uteuzi wa Kardinali Rugambwa ni kielelezo na ushuhuda wa ukweli kwamba Tanzania ni nchi ya amani na imekuwa na bahati ya kuwa na Kardinali ambaye ni wa tatu baada ya Laurean Kardinali Rugambwa na Kardinali Pengo.

“Rais Samia Suluhu Hassan yuko nje ya nchi kikazi na anatarajia kwenda India kwa  ziara ya kikazi.  Kwa  niaba yake, serikali na Watanzaia karibu nyumbani. Tumefurahi  tumepata baraka kama ulivyosema. Ni  baraka kubwa kwa nchi yetu,” alisema Dk. Mpango.

Alisema kwa mara ya tatu wamejaliwa kupata Kardinali na wanaamini kwa Tanzania wanaposema wana amani ni kutokana na mambo mazuri kama hayo ambayo Mungu anaendelea kuyakirimia.

Kwa niaba ya serikali, alisema wanampongeza na wanachozidi kuomba ni amani ya taifa walimfuatilia alivyokuwa Vatican nchini Italia aliendelea kusisitiza amani na umoja kwa Watanzania.

“Katika nafasi hii mpya sijajua wataendelea kukuweka Tabora, sijui watakuweka wapi. Lakini  tunaamini kabisa utaendelea kuwa chumvi ya amani, umoja na upendo kwa Watanzania,” alisema.

Aidha, alisema Rais Samia atakaporejea nchini atafanya utaratibu wa kumkaribisha nyumbani kwa kuwa ni mkuu wa nchi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Evelyne  Ntenga, alisema wanaendelea kumuombea kwa Mungu ili kazi aliyoipokea aifanye kwa uadilifu.

Alitaka wanawake watenge muda na kukaa na watoto ili kuwasaidia kile ambacho Mungu amekiweka ndani yao ili wawe na maadili mema.