Rais Samia atoa gari Morogoro kusaidia kupunguza vifo vya watoto

09Feb 2024
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Rais Samia atoa gari Morogoro kusaidia kupunguza vifo vya watoto

RAIS Samia Suluhu Hassan,ametoa gari la kubebea wagonjwa katika Hospitali ya wilaya ya Morogoro kwa lengo la kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto ambavyo vimekuwa tishio kwa sasa.

Akikabidhi gari hilo,Mbunge   wa Jimbo la Morogoro Mjini Abdulaziz Abood ,amesema ni  la pili kutolewa  kwaajili ya  kubebea wagonjwa  (Ambulance) kwa wilaya ya Morogoro  huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza maombi yake.

Abood alisema Rais Samia alitoa gari la kwanza la kubebea  wagonjwa  katika kipindi cha miezi miwili iliyopita katika  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo.Abood, amesema litasaidia wakazi wa Manispaa ya Morogoro kuendelea kupata huduma bora za afya huku akimpongeza Rais Samia  kwa kusikiliza ombi lake  kwa ajili ya  Hospitali hiyo ya wilaya ambayo inahudumia wakazi wengi wa Manispaa ya Morogoro.

Amesema Hospitali hiyo ya wilaya ambayo inaendelea kujengwa imekuwa ikakabiliwa na ukosefu wa gari la wagonjwa hasa pale kina mama wajawazito na watoto wanaopewa rufaa kwenda katika hospitali ya rufaa ya mkoa.

“ Namshukuru kwa dhati kabisa Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kwa kukubali ombi langu la gari la wagonjwa katika hospitali hii ya wilaya,alishanipa gari la kwanza katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa lakini kulikuwa na changamoto katika hospitali  hii hasa pale wakinamama wajawazito na watoto wanapopewa rufaa “ amesema Abood.

Amesema pamoja na wajawazito lakini pia wananchi wa Morogoro mjini ambao  walikuwa wakipata changamoto  ya usafiri wakipewa rufaa ya kutoka kwenye vituo vya afya kwenda Hospital  ya Rufaa ya Morogoro.

"Namshukutu sana  Rais Samia Hassan Suluhu  kwani amekuwa msikivu kila ninapomuomba kutatua changamoto  za wana Morogoro mjini, ametoa fedha nyingi katika ujenzi wa Miradi ya afya, ununuzi wa vifaa na vifaa tiba vya kisasa na huduma za dawa kwa ajili ya kutolea huduma katika Jimbo la la Morogoro mjini." amesema Abood

Mbunge huyo alichukuwa nafasi hiyo kuwapongeza Madaktari na wahudumu wote wa afya katika hospitali ya wilaya, divisioni ya afya na maendeleo ya Jamii sambamba na viongozi wa Halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi wa manispaa kwa kazi nzuri wanazozifanya kwenye idara hiyo.

 Naye Mkurugenzi  wa Manispaa  ya Morogoro Ally Machela,amemuhakikishia Mbunge huyo kuwa gari zote za wagonjwa zilizotolewa na Rais Samia pamoja na Mbunge huyo  zitatunzwa kikamilifu kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili wagonjwa.

Amechukuwa nafasi hiyo kumpongeza Mbunge Abood kwa jitihada mbalimbali anazofanya kwaajili ya kupigania Manispaa ya Morogoro kupata maendeleo.