Rais Samia aonya walioanza kampeni

06Feb 2022
Na Waandishi Wetu
Musoma
Nipashe Jumapili
Rais Samia aonya walioanza kampeni

​​​​​​​CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza utaratibu mpya wa kuadhimisha sherehe za kuzaliwa kwake kitaifa wa kila baada ya miaka mitano, huku Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan akitoa onyo kwa wanachama walioanza kampeni mapema.

Rais Samia alitoa onyo hilo jana mjini Musoma mkoani Mara wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 45 tangu kuzaliwa kwa chama hicho, akisema sherehe hizo kwa kila mwaka zitakuwa zinaadhimishwa kimkoa.

Alisema uchaguzi ndani ya chama utafanyika mwaka huu na kubainisha kuna watu wameanza harakati za kutaka uongozi mkoani Mara kabla ya muda.

Alisema jicho la chama lipo wazi kwa wanaoanza kampeni kabla ya muda.

Rais Samia alisema chama hicho kilifanya matembezi ya hisani na kukusanya Sh. milioni 300 ambazo ameelekeza zitumike kutengeneza kadi  za kielektroniki.

Kiongozi huyo pia alibainisha mafanikio katika sekta mbalimbali zikiwamo kilimo  na kupongeza Tanzania kufikia uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025.

Sherehe hizo zilifanyika kwa mara ya pili mkoani Mara tangu kuzaliwa CCM, zilihudhuriwa na makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho na viongozi wengine wa kitaifa wakiamo Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson.

*Imeandikwa na Richard Makore na Beatrice Shayo