Prof. Carolyne Nombo ataka ushirikiano mabadiliko sekta ya elimu

03Mar 2024
Halfani Chusi
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Prof. Carolyne Nombo ataka ushirikiano mabadiliko sekta ya elimu

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Carolyne Nombo amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na taasisi zake ili kuleta mabadiliko endelevu katika sekta ya elimu kwa ujumla.

Kiongozi huyo aliyemwakilisha Waziri wa Elimu wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda aliyasema hayo jana jijin Dar es Salaam alipofungua kongamano la Elimu Bila Ukomo mwaka 2024.

Carolyne alisema, serikali ya imeweka dhamira ya dhati ya kuendeleza elimu nchini, akisisitiza hilo limedhihirika kutokanana na kukamilika kwa zoezi la maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, pamoja na mitaala. 

"Sisi kama wizara tunaona fahari kubwa kwa kazi kubwa iliyofanyika na tuna imani kuwa utekelezaji wa mabadiliko yaliyofanyika utaleta mapinduzi ya kielimu na kijamii nchini. 

"Mabadiliko ya mitaala hayapaswi kuishia kwenye mfumo rasmi pekee yanatakiwa pia katika sekta ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi vilevile" alisema

Alisema Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, pamoja na malengo mengine imelenga kukuza fursa za elimu isiyo na ukomo kwa watu wote, na kujenga Watanzania mwenye utamaduni wa kupenda kujisomea na kujiendeleza katika muktadha huo. 

Alikumbushia kuwa sera hiyo pia inatoa msimamo kwamba. Elimu nje ya mfumo rasmi itatambuliwa na watakaopitia mfumo huo watakuwa na fursa ya kujiunga na mfumo rasmi wa elimu kulingana na vigezo vitakavyowekwa. 

Alifafanua kwamba sera imeweka hakikisho kuwa Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, itaendelea kuimarisha na kusimamia afua mbalimbali zinazolenga kutoa fursa za elimu kwa wale walioikosa. 

"Katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, dhana inayotawala ni ile ya elimu bila ukomo, kwa hiyo, elimu ya watu wazima inapewa nafasi kubwa zaidi, inaandaa jamii kupata stadi za msingi za kujua kusoma, kuandika na kuhesabu, na stadi za maisha.

“Inatoa fursa ya kuwa na jamii inayojali na kuthamini elimu, kwa kuhakikisha watoto wanaandikishwa na kuwawezesha kufanya vizuri katika masomo, pia inatoa fursa kwa walioikosa ili kupata elimu kupitia elimu nje ya mfumo rasmi” alisema Prof Calolyne

Aliwataka waliohudhuria Katika kongamano hilo kufanya mjadala mpana wa kitaifa ili kupata mawazo ya namna bora ya kutekeleza shughuli za Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, sambamba na mabadiliko ya Sera mpya ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023.

Alisema kwa Sasa Serikali inataka elimu ya watu wazima ilenge mabadiliko ya sayansi na teknolojia na mtazamo wa sasa, kama ulivyosisitizwa katika sera mpya ya elimu.

"Ndugu Mwenyekiti wa Kongamano, Kwa kuzingatia kaulimbiu ya kongamano hili, Mabadiliko ya Sera ya Elimu nchini, Fursa na Changamoto katika Utoaji wa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, nimefurahi kuwa mjadala wetu utachokozwa na wawasilisha mada waliobobea katika maeneo yao ya taaluma na utaalam. 

"Nimefurahi mada zimeandaliwa kuvutia mjadala katika maeneo ya kisheria, muundo wa kitaasisi, uzoefu kutoka nchi zingine na ushiriki wa sekta binafsi na asasi za kiraia. Maeneo haya ni muhimu ili kuwa na elimu ya watu wazima yenye mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya taifa” alisema

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Prof Michael Ng’ubi alisema elimu bila ukomo itamwezesha Mtanzania kusoma tangu anapozaliwa mpaka mwisho wa maisha yake.

“Wajibu wa wananchi ni kubadilisha mtazamo hakuna tofauti kati ya kusoma na kuishi ilizoweleka kwamba mtu akifikia kiwango Fulani Cha elimu anaachwa kusoma ananza kutafuta maisha.

“Na ndio maana hapa Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima tunakwenda kutengeneza miongozo na utaratibu utakaompa mwanafunzi fursa ya kuendelea kijifunza muda wote” alisema Prof Ng’umbi