Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa wakati akikabidhi magari matatu yaliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya jeshi hilo ili kukabiliana na uhalifu.
Malisa alisema suala la usalama wa raia na mali zao sio la polisi pekee bali ni la kila mwananachi, hivyo kuna umuhimu mkubwa kushirikishwa kukabiliana na uhalifu.
“Tunahitaji kuifanya jamii yetu iishi kwa amani na utulivu, lakini ili tufanikiwe ni lazima wananchi washirikishwe kwa kupewa elimu ya kukabiliana na uhalifu, Polisi msitumie nguvu pekee kukabiliana na uhalifu bali waelimisheni wananchi ndipo tutafanikiwa,” alisema Malisa.
Alisema utaratibu wa sasa wa Jeshi la Polisi kupeleka askari katika kila kata ni mzuri kwa kuwa wakichangamana na jamii wanaweza kuzuia uhalifu kabla haujatokea na kuifanya jamii iishi kwa amani na utulivu.
Akipokea magari hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema yatalisaidia jeshi hilo kufanya kazi kwa weledi wakati wa kukabiliana na wahalifu.
Kuzaga alisema kupatikana kwa magari hayo kutaongeza vitendea kazi kwa askari wa jeshi hilo kwa kuyatumia kufika maeneo mbalimbali kwa wakati kudhibiti uhalifu.
“Magari haya yatatufanya tuwahi kwenye maeneo yenye viashiria vya kutokea uhalifu na kuvidhibiti,” alisema.
Alisema anaamini kuwa utafika wakati ambao wilaya zote za mkoa wa Mbeya zitakuwa na magari mapya ambayo yatatumika kudhibiti uhalifu kwa wakati mpaka maeneo ya vijijini.
Alisema mwaka huu jeshi hilo mkoani hapa limejipanga kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili washirikiane kudhibiti uhalifu na wahalifu kwa lengo la kuifanya jamii iishi kwa amani na utulivu.










