Inadaiwa kuwa Jennifer alikuwa na tabia za kutoweka nyumbani kwa zaidi ya mwezi mmoja lakini tangu alivyotoweka Machi 2020, hajarudi hali iliyosababisha wanafamilia kuwa na shaka na mume wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi (ACP) Safia Jongo, alisema walipata taarifa ya tukio hilo, wakafuatilia kibali cha Mahakama ili kujiridhisha juu ya uwapo wa mwili ndani ya nyumba ya wanandoa hao. Hata hivyo, walipoingia ndani ya nyumba hiyo hawakuupata.
“Aprili 3, mwaka huu, tulipata kibali tukaanza kufukua, tulifanikiwa kufukua mashimo manne yaliyokuwa yanahisiwa na ndugu hao. Mpaka inafika usiku hatukupata matokeo yoyote. Tukarudi Aprili 5 na kufukua maeneo yaliyokuwa yanashukiwa kadhalika hatukuupata mwili wa mwanamke huyo. Kwa hiyo familia na wenyewe wakathibitisha kwamba hakuna mwili uliofukiwa,” alisema Jongo.
Kamanda Jongo alisema kwa sababu za kiuchunguzi na usalama, imewalazimu kumshikilia mwalimu huyo ili kumwepusha na watu wanaomtishia maisha.
"Tunahofia usalama wake kwahiyo uchunguzi utakapokamilika wale ambao wanatishia usalama tutawachukulia hatua lakini huyu mwalimu bado tunamhifadhi kwa ajili ya usalama wake”, alisema Jongo.
Aidha, Kamanda Jongo alisema kutokana na jeshi hilo kupokea taarifa hizo rasmi, watafanya utaratibu wa kuendelea kumtafuta kwa kuzitangaza picha zake kwenye kwenye vyombo vya habari ili kama bado yuko hai na yuko mahali kupatikana na hatua zaidi zichukuliwe.
Kwa mujibu wa Kamanda Jongo, walimhoji mama wa Jennifer ambaye alikiri kwamba mtoto wake alikuwa na tabia ya kuondoka nyumbani akigombana na mume wake na kurudi baada ya mwezi au miezi mitatu.
Alisema lakini imekuwa tofauti kwa kipindi hiki kwa kuwa tangu aondoke Machi 2020, hakuwahi kurudi hali iliyosababisha ndugu hao kuhisi mtoto wao ameuawa na mume wake na kuzikwa ndani ya nyumba.










