Ibara ya 14 ya Katiba hiyo iliyotungiwa Sheria Na. 15 ya Mwaka 1984 (Haki ya Kuishi) inatamka bayana kwamba "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria".
Huku kukiwa na angalizo hilo la kikatiba na kisheria, sasa kunashuhudiwa idadi kubwa ya matukio ya mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi wanandoa na wapendanao wengine wakitoana roho kila kukicha.
Kwa kurejea matukio machache, Mei 28 mwaka huu huko Buswelu mkoani Mwanza, binti wa miaka 28 aliuawa na mumewe kwa kupigwa risasi kwa madai yaleyale ya wivu wa mapenzi. Saa chache baadaye, ikaripotiwa na Jeshi la Polisi kwamba mumewe naye amejiua kwa kujipiga risasi baada ya kutekeleza mauaji dhidi ya mkewe.
Mkoani Shinyanga nako kumeripotiwa tukio la mwanamke kudaiwa kumjeruhi mumewe kwa kumkata sehemu za faragha kwa tuhuma za usaliti.
Huko Tunduru mkoani Ruvuma, mwanamke ameripotiwa na Jeshi la Polisi kufariki dunia na kuacha mtoto wa miezi 11, akidaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi kichwani na mchumba wake kutokana na sababu ileile wivu wa mapenzi.
Tukio la mauaji ya aina hiyo pia limetokea wilayani Butiama mkoani Mara, mwanamke mwingine akiripotiwa kumuua mumewe kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha kali kwa tuhuma za usaliti.
Hali kadhalika, wilayani Serengeti mkoani Mara ilitolewa taarifa na Jeshi la Polisi ya mume kudaiwa kumjeruhi mkewe kwa kumwingiza panga sehemu za siri, akimtuhumu kuwa na uhusiano na mwanamume mwingine.
Jeshi la Polisi pia limeripoti tukio la mwanamke kumjeruhi mumewe kwa kumkata na wembe sehemu za siri akiwa usingizini na kumsababishia maumivu makali mkoani Ruvuma.
Sasa inaonekana ni matukio endelevu, huku kitendawili kikibaki kuwa 'kuna nini nyuma ya ukatili huu? Pia, kwa nini sasa yanashamiri nchini?
NYUMA YA PAZIA
Nipashe Jumapili inatua mezani kwa Zainabu Rashid, mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii mkoani Dar es Salaam, anayepaza sauti dhidi ya migogoro ya wapendanao isiyotatuliwa.
Zainabu ana ufafanuzi, akitamka: "Sababu inaweza kuwa ni mrundikano wa migogoro. Mtu anapolimbikiza matatizo, yale matatizo ni kama kidonda, kile kidonda usipokitibu kwa wakati kinaendelea kukua na kinapokua, mwisho wa siku kinaweza kukuletea madhara.
"Inapotokea mume amemkosea mke wake au mke amemkosea mume wake kwa muda mrefu na amekaa bila kusuluhisha jambo hilo, inatengeneza kama kidonda kinakua.
"Kitakapolipuka, akili ya binadamu ina namna fulani ya kufanya kazi kulingana na vile ulivyotunza taarifa. Hivyo, mtu anaweza kufanya jambo bila kujua, lakini ni matokeo ya uzoefu alioupata baada ya kufanya jambo fulani.
"Kuna kitu kinaitwa haiba, mwingine anaweza kusamehe, mwingine ni rahisi kusahau, mwingine anatunza. Mwisho wa siku anakuja kufanya tukio kubwa kwa sababu ametunza matukio mbalimbali.
"Kitu kingine ni malezi, hasa ya kihisia. Familia nyingi hazilei watoto katika ukuaji wa kihisia katika kuhimili hisia zao, kwa sababu siyo kila haki yake atapewa. Kwa hiyo, wanandoa au wapenzi wanaingia kwenye mauaji kwa sababu wameshindwa kuhimili hisia zao za hasira au wivu."
Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, hayuko mbali katika kukimulika kilicho nyuma ya pazia kuhusu mauaji miongoni mwa wapendanao.
Kiongozi huyo wa kiroho anasema: "Ni wimbi tu la shetani linapita, kwa sababu mambo kama haya huwa yanatokea kwa kipindi fulani kisha yanapotea. Lakini kama ni elimu, viongozi tunatoa juu ya uharamu wa kujiua na kuua mtu mwingine."
Akiwa mkoani Iringa juzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, alilaani vitendo vya mauaji vinavyofanywa na baadhi ya watu kwenye jamii, yakiwamo yanayohusisha wapendanao.
Alisema jeshi hilo litaendelea kuwachukulia hatua za kisheria watu watakaobainika ikiwamo kuwafikisha mahakamani, akisisitiza kuwa kumekuwa na matukio ya mauaji aliyoyaita ya ovyo ambayo yanasababishwa na ukosefu wa maadili na hata imani za kishirikina.
"Tufike mahali tuseme basi, tujue kuwa Mungu yupo na kwamba kuna siku tutakwenda kuwajibika," IGP Sirro alionya.
NINI KIFANYIKE?
Ili kukabiliana na tatizo hilo, Mwanasaikolojia Zainabu ana angalizo kwa wazazi na walezi kuwa chimbuko la mauaji haya miongoni mwa wapendanao ni makosa yaliyochagizwa na wazazi na walezi kutowajibika katika malezi ya watoto wao.
"Wazazi wazingatie malezi ya ukuaji wa watoto kihisia, watoto wanakua na hisia tangu wanapozaliwa. Kwa hiyo, mpaka wanapokuwa watu wazima, watakuwa wanajua namna ya kuhimili hisia zao," anasisitiza.
Mwanasaikolojia huyo pia ana rai yake kwa jamii, akiitaka kuchukua hatua inapoona mtoto anakwenda kinyume cha maadili mema yaliyowekwa kwenye jamii anayoishi.
Nipashe Jumapili inaporejea kwa Shekhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum, kupata mustakabali wa tatizo la mauaji yanayotikisa ya wapendanao nchini, anashauri:
"Inawezekana hata mawaidha yanayotokana na viongozi wa dini siyo watu wote yanawafikia huko maeneo waliko. Kwa hiyo, inatakiwa kuongeza vyombo vya mawasiliano katika vijiji, kwenye miji mbalimbali na watu wawe wanafuatilia vyombo hivi ambavyo vitawaelimisha kwa namna moja au nyingine.
"Pia watu wafuate misingi yao ya dini na miongozo yao ya kiimani ili kujiepusha na majaribu ya shetani."
Ni muhimu wanandoa wawe wepesi kujifunza, kujikosoa, kujisahihisha na kuombana msamaha pale mtu anapohisi kumkosea mwenzake. Ni vema ifahamike kuwa, hakuna ndoa yenye afya njema bila zoezi la msamaha. Msamaha ni dawa ya furaha ya familia. Msamaha ni muhimu kwa afya yetu ya kihisia na kuendelea kuishi kwa heri. Asiyeomba msamaha na asiyesamehe hana amani katika nafsi yake na hawezi kuwa na ushirika na Mungu. Pia, mtu wa aina hiyo hawezi kuwa na uhusiano mwema na binadamu mwenzake.
Watu wasioomba msamaha na wasiosamehe ni wagonjwa wa kimwili, kihisia na kiroho. Siku zote huteseka na kuishi kwa vinyongo na roho ya visasi na maangamizi. Bila msamaha, familia inakuwa uwanja wa migogoro, ngome ya uovu na maafa.
Mchungaji wa Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania (KKKT), Dk. Mlyuka, anasema migogoro ya ndoa ni adui wa maendeleo kwa kuwa maendeleo na ustawi wa familia na Taifa unategemea ndoa imara.
Dk, Mlyuka ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Marriage and Child Care (TaMCare) inayojishuhulisha na masuala ya ndoa, familia na malezi, anasema ni muhimu kila mwanandoa ajiheshimu, atambue nafasi, wajibu na mipaka yake katika ndoa ili kuifanya ndoa kuwa baraka.
Vilevile, IGP Sirro katika kusaka mwarobaini wa mauaji miongoni mwa wanandoa na wapendanao, hayuko nyuma kuishauri jamii, akitamka: "Kama unaona mwanamke amekuzingua, unaachana naye. Pia, kama mwanamume amekuzingua, unaachana naye, maisha yanaendelea kama kawaida.
"Na pia kinadada muangalie ni mwanaume gani unaolewa naye, siyo kila mwanamume ni mwanamume bora, kuna wanaume wengine ni mizigo na kuna wanawake wengine ni mizigo pia."
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilirekodi matukio ya mauaji ya kikatili 20, yakiwamo ya wapendanao, kwa mwezi Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Anna Henga, matukio hayo yaliripotiwa katika mikoa ya Mtwara, Rukwa, Njombe, Katavi, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Dar es Salaam na Mara.
*Imeandaliwa na Joyce Ammi, Lydia Sylivester na Wilbgeorge Bahati (SJMC).










